KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 23, 2011

MICHELLE JENG: NAPENDA KUSAIDIA WATOTO WENYE MATATIZO




Ni mshindi wa taji la Miss Africa Scandinavia 2010

Anasomesha watoto yatima wawili hapa Bongo

Aliwahi kupanda Mlima Kilimanjaro hadi kileleni

MSHINDI wa taji la ‘Miss Africa Scandinavia 2010’, Michelle Jeng amesema atalitumia taji hilo kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu hapa nchini.
Akihojiwa katika kipindi cha Jambo cha kituo cha televisheni cha TBC 1 mwishoni mwa wiki iliyopita, Michelle alisema siku zote yeye ni mtu anayependa kusaidia watu wenye matatizo.
Michelle (19), ambaye alishinda taji hilo mwishoni mwa mwaka jana nchini Sweden, alisema tayari ameshaanza kutoa misaada mbalimbali kwa watoto walioathirika katika milipuko ya mabomu iliyotokea kwenye kambi ya jeshi iliyopo Gongo la Mboto mjini Dar es Salaam.
Mrembo huyo alisema, alikabidhi misaada hiyo wiki iliyopita kwa Kaimu Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Mecky Sadiki.
Michelle ni mzaliwa wa Sweden. Mama yake ni mtanzania wakati baba yake ni raia wa Gambia.
Kwa mujibu wa Michelle, alikusanya vitu alivyomkabidhi mkuu huyo wa mkoa kutoka kwa watanzania mbalimbali wanaoishi na kufanyakazi nchini Sweden.
Mbali na misaada huyo, Michelle pia amejitolea kuwasomesha watoto wawili, ambao ni yatima. Alianza kuwasomesha watoto hao tangu akiwa shule ya sekondari mwaka 2005.
Alisema kwa sasa, mmoja wa watoto hao anasoma kidato cha pili katika shule moja ya sekondari mkoani Dodoma na mwingine yupo darasa la tatu katika shule moja ya msingi mjini Arusha.
Michelle, ambaye amekuwa akija nchini mara kwa mara, alisema aliwaona watoto hao mwaka huo wakati yeye na mama yake walipokuja nchini na kumtembelea mmoja wa marafiki zake.
“Unajua kusaidia kwa kutoa tu haitoshi, ni vizuri ukimsaidia mtu kwa ajili ya maisha yake ya baadaye, hasa kwa kumpatia elimu,”alisema mrembo huyo, ambaye aliwahi kupanda Mlima Kilimanjaro mwaka jana na kufanikiwa kufika hadi kileleni.
Mrembo huyo alisema amekuwa akiwalipia pesa za ada watoto hao kutokana na malipo ya kazi za muda, ambazo amekuwa akizifanya kila mwisho wa wiki. Alisema wanafunzi nchini Sweden wanaruhusiwa kufanyakazi mwisho wa wiki.
Alisema pesa zingine zinatokana na posho, ambayo amekuwa akiipata kutoka kwa serikali ya Sweden na zingine zinatokana na mikopo, ambayo amekuwa akichukua kwa ajili ya kujiendeleza.
Kwa mujibu wa Michelle, kila mtoto anayezaliwa Sweden, analipwa posho kwa ajili ya kumsaidia kielimu. Alisema lengo lake ni kuona watoto hao wawili wanafika chuo kikuu.
Alisema uamuzi wake wa kuwasaidia watoto hao umetokana na tofauti ya kimaisha aliyoiona kati ya watoto wanaoishi Sweden na wale wanaoishi katika nchi za Kiafrika.
Mrembo huyo, anayejiandaa kuingia chuo kikuu alisema, anapenda kusomea udaktari kwa vile lengo lake kubwa katika siku zijazo ni kutoa huduma ya afya, hasa kwa watoto.
“Kwa sasa nimemaliza kidato cha sita, najiandaa kuingia chuo kikuu mwakani. Nataka nitakaporudi Afrika, niwe daktari ili niwasaidie watoto na nchi yangu. Afya ni kitu muhimu. Kila mtu anayo haki ya kupatiwa matibabu,”alisema.
Michelle alishinda taji la Miss Africa Scandinavia baada ya kuwabwaga warembo wengine 20 kutoka nchi mbalimbali za Afrika. Washiriki wengine walitoka nchi za Tanzania, Togo, Cameroon, Kenya, Uganda, Sierra Leone na Gambia.
Mrembo huyo anaamini kuwa, alishinda taji hilo kutokana na kujiamini kwake, kujikubali jinsi alivyo, kutokuwa na makuu na pia kupenda kusaidia wengine.
Alisema kwa kawaida, uzuri wa mtu upo ndani yake kwa vile haujionyeshi wazi. Alisema cha msingi ni kuwafikiria na kuwasaidia watu wengine wenye matatizo.
Michelle alisema mama yake alimsaidia kwa kumpa moyo wakati wote wa maandalizi, ikiwa ni pamoja na kumtafutia nguo za Kitanzania, ambazo alizivaa wakati wa shindano hilo.
Akizungumzia hilo, mama wa mrembo huyo, anayejulikana kwa jina la Nuru alisema: “ Kila anachotaka kukifanya, huwa nampa moyo. Katika maisha ni vizuri kujaribu, usishindwe kujaribu.”
Michelle, ambaye atatimiza umri wa miaka 20 ifikapo Novemba mwaka huu alisema, hajui lolote kuhusu mashindano ya kumsaka mrembo wa Tanzania zaidi ya kusoma habari zake kupitia kwenye tovuti mbalimbali.
“Sijawahi kuyashuhudia mashindano haya wala kukutana na waliowahi kushinda taji hili. Napenda kufahamu mengi kuhusu shindano hili,”alisema.
Mrembo huyo alisema, japokuwa washindi wa taji hilo hawakuwahi kufanya vizuri katika shindano la dunia, wamekuwa wakiitangaza vyema nchi yao kimataifa. Alisema kushinda ni matokeo.
Ametoa mwito kwa wasichana wa Tanzania wanaojihusisha na fani ya urembo, waitumie vyema kujinufaisha katika maisha yao badala ya kuichukulia kuwa ya kihuni.
“Si jambo zuri kwa mrembo wa Tanzania kujikweza, wasipende kujiremba kupita kiasi, waringie rangi zao za asili. Mrembo anatakiwa kuwa mtu wa kusaidia watu wenye matatizo, awe na busara na hekima,”alisema.
Michelle alisema binafsi anaichukulia fani ya urembo kama burudani kwa vile hatarajii kujihusisha nayo kwa maisha yake yote. Alisema kwake, anachokipa kipaumbele zaidi ni masomo, hasa kuwa daktari.

No comments:

Post a Comment