KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 23, 2011

Fabregas, Nasri waitega Arsenal


LONDON, England
WACHEZAJI Samir Nasri na Cesc Fabregas wa klabu ya Arsenal ya England wameendelea kumuumiza kichwa kocha mkuu wa timu hiyo, Arsene Wenger baada ya kushindwa kuweka wazi kuhusu mustakabali wao.
Wakati Fabregas amekuwa akiwindwa vikali na klabu yake ya zamani ya Barcelona ya Hispania, Nasri anaonekana kumtega Wenger baada ya kugoma kutia saini mkataba mpya.
Nasri alisema wiki hii kuwa, hawezi kutia saini mkataba mpya hadi atakapoona klabu hiyo itatumia kiasi gani cha pesa kwa ajili ya kusajili wachezaji wapya msimu ujao.
Gazeti la Times la Uingereza liliripoti kuwa, Nasri amesema atakuwa tayari kutia saini mkataba mpya iwapo atahakikishiwa kuwa, kikosi cha Arsenal kitaimarika zaidi msimu ujao.
Kiungo huyo aliweka wazi kuwa, iwapo atapata ofa nzuri kutoka katika klabu zingine, atakuwa tayari kuondoka Arsenal kwa vile lengo lake ni kutwaa mataji mengi.
Nasri alisema hadi sasa hana hakika iwapo atatia saini mkataba mpya katika klabu hiyo yenye maskani yake kwenye uwanja wa Emirates.
Kuna habari kuwa, Nasri amekuwa akiwindwa na klabu ya Manchester United, lakini Kocha Wenger hataki kumuuza licha ya kubakisha mwaka mmoja kwenye mkataba wake.
Hivi karibuni, beki Patrice Evra wa Manchester United alimtaka mchezaji huyo ajiunge na klabu hiyo kama anataka kutwaa mataji mengi katika kipindi chote atakachocheza soka England.
Uamuzi wa Nasri kukataa kutia saini mkataba mpya na Arsenal umezusha hisia kuwa, huenda kiungo huyo wa kimataifa wa Ufaransa anataka kuhama.
Akihojiwa na kituo cha radio cha TF1’s Telefoot cha Ufaransa hivi karibuni, Nasri alisema atakuwa tayari kujiunga na Manchester United iwapo klabu hiyo itamuhitaji.
“Nataka kwenda Manchester United? Tusubiri tuone kama itakuwa kweli,”alisema Nasri.
Mchezaji huyo alisema kwa sasa hawezi kutoa uamuzi wowote mpaka Ufaransa itakapocheza na timu za Ukraine na Poland katika mechi za kuwania kufuzu fainali za Ulaya za mwaka 2012.
“Sielewi iwapo nitatia saini mkataba mpya. Mazungumzo bado yanaendelea. Kwa sasa, sifikirii kuhusu hili. Tutalizungumza baada ya mechi dhidi ya Poland,”alisema.
Imeelezwa kuwa, Kocha Sir Alex Ferguson wa Manchester United anahaha kusaka kiungo mpya, kufuatia kustaafu kwa Paul Scholes wakati Wenger hayupo tayari kuona mchezaji wake anahamia kwa mahasimu wao.
Gazeti la Daily Mail la Uingereza lilimkariri Wenger hivi karibuni akisema: “Kitu kimoja cha uhakika, hatuwezi kumuuza kwa Manchester United.”
Wenger alielezea msimamo wake huo baada ya kuulizwa kuhusu mustakabali wa Nasri.
Mbali na kumnyemelea Nasri, kuna habari kuwa Ferguson pia anamuwinda kiungo Wesley Sneijder wa klabu ya Inter Milan ya Italia.
Kiungo huyo wa kimataifa wa Uholanzi pia anawindwa na klabu ya Manchester City, ambayo imetenga pauni milioni 30 za Uingereza kwa ajili ya kumsajili.
Wakala wa Nasri, Alain Migliaccio alikaririwa hivi karibuni akisema kuwa, mazungumzo kati yake na Arsenal kuhusu mkataba mpya wa mchezaji huyo hayajavunjika.
“Kabla ya kuzisikiliza timu zingine, tunahitaji na tunataka kuzungumza na Arsenal,”alisema wakala huyo.
Wakati huo huo, Wenger amesema hawezi kumuuza Fabregas kwa klabu ya Barcelona, licha ya klabu hiyo kuwasilisha ofa yenye dau kubwa.
Wenger ameelezea msimamo huo baada ya Barcelona kuwasilisha tena maombi ya kumsajili Fabregas kwa klabu ya Arsenal.
Kwa upande wake, Fabregas amesema anafurahia kuwepo Arsenal na kusisitiza kuwa, hawezi kuiumiza klabu hiyo.
“Siwezi kujitokeza mbele na kusema nataka kujiunga na Barcelona. Baada ya miaka minane Arsenal, siwezi kuiumiza klabu. Hiyo siyo desturi yangu,”alisema.
“Nina furaha kubwa kuwepo hapa. Mimi ni mchezaji wa Arsenal kwa sasa. Zilizobaki ni tetesi. Wenger anafahamu nini ninachokitaka nay eye ni bosi, anaamua,”aliongeza.
Barcelona imekuwa ikihaha kumsajili mchezaji huyo tangu msimu uliopita na hivi karibuni iliweka wazi kuwa, itamuuza mshambuliaji wake David Villa kwa Chelsea ili ipate pesa za kumsajili Fabregas.
Mabingwa hao wa ligi ya Ulaya pia wana matumaini ya kumsajili winga Alexis Sanchez kutoka Udinese ya Italia na mshambuliaji Giuseppe Rossi kutoka Villarreal ili kukiimarisha zaidi kikosi chao.
Hata hivyo, bajeti ya Barcelona ya kusajili wachezaji wapya ni pauni milioni 40, hivyo inataka iongeze fedha zingine kwa kumuuza Villa.
Villa (29), ambaye alijiunga na Barcelona msimu uliopita, akitokea Valencia, huenda akauzwa Chelsea, ambayo inahaha kusaka mshambuliaji mpya.
Awali, Chelsea ilikuwa ikitaka kumsajili Neymar kutoka Brazil, lakini mshambuliaji huyo aliamua kujiunga na Real Madrid. Kwa sasa, lengo kubwa la Chelsea ni kumnasa Villa, ambaye ana uzoefu wa kucheza pamoja na Fernando Torres.
Gazeti la Daily Mail lilimkariri Kocha Pep Guardiola wa Barcelona akisema kuwa, angependa kumbakisha Villa, hasa baada ya kuwa na msimu mzuri, lakini atakuwa tayari kumuuza kwa lengo la kukiimarisha zaidi kikosi chake.

No comments:

Post a Comment