'
Wednesday, June 15, 2011
Sikinde sasa hakuna kulala
BENDI ya muziki wa dansi ya Extra Bongo na kikundi cha muziki wa kiasili cha Segele, vitatoa burudani katika onyesho la uzinduzi wa vyombo vipya vya Mlimani Park Orchestra.
Katibu wa Mlimani Park ‘Sikinde’, Hamisi Milambo alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, onyesho hilo limepangwa kufanyika Juni 25 mwaka huu.
Milambo alisema tayari Extra Bongo, inayoongozwa na Ally Choki pamoja na Segele, zimeshathibitisha kuisindikiza Sikinde katika onyesho hilo litakalofanyika kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Milambo, vyombo hivyo vyenye thamani ya sh. milioni 45,vimetolewa na Kampuni ya Vinywaji ya Konyagi, ambayo ni wadhamini wakuu wa Sikinde.
“Kwa sasa, Konyagi ndio wadhamini wakuu wa Sikinde na wameamua kutupatia vyombo hivyo kwa lengo la kuuboresha zaidi muziki wetu,”alisema.
Katibu huyo wa Sikinde alisema, wamepanga kuvionyesha vyombo hivyo kwa waandishi wa habari Juni 21 katika mkutano utakaofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani Park, uliopo Mwenge, Dar es Salaam.
Mbali na kuzindua vyombo vipya, Milambo alisema watalitumia onyesho hilo kumtambulisha rasmi mwimbaji wao mpya,Athumani Kambi, aliyejiunga na bendi hiyo hivi karibuni akitokea Vijana Jazz.
Vilevile alisema watalitumia onyesho hilo kuzitambulisha nyimbo zao nne mpya. Alizitaja nyimbo hizo kuwa ni Jinamizi la talaka, Mihangaiko ya kazi, Deni nitalipa na Kinyonga.
“Tumeamua kumtambulisha rasmi Athumani Kambi siku hiyo kwa sababu ndiye atakayekuwa mrithi wa Hassan Bitchuka kwa vile ana uwezo wa kuimba nyimbo zote za zamani za mwimbaji huyo na ndiye atakayemkabidhi kipaza sauti,”alisema.
Milambo amewataka mashabiki wa Sikinde kujitokeza kwa wingi katika onyesho hilo kwa sababu wataibuka kivingine, wakiwa na mambo mpya. Alisisitiza kuwa,wanamuziki wa Sikinde hivi sasa wameamua hakuna kulala.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment