KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 9, 2011

BASENA: Motema Pembe 'Kushnei'



Na Sophia Wakati, Tanga
KOCHA Mkuu wa Simba, Moses Basena amesema kikosi chake kimeiva na kipo tayari kuikabili DC Motemba Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo katika mechi ya mtoano ya michuano ya soka ya Kombe la Shirikisho.
Simba na DC Motema Pembe zinatarajiwa kushuka dimbani Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kurudiana wiki mbili zijazo mjini Kinshasa.
Akizungumza mjini hapa juzi, Basena alisema kambi ya timu hiyo inaendelea vizuri na wachezaji wake wote wapo fiti, isipokuwa kipa Juma Kaseja, ambaye bado majeruhi.
Kaseja aliumia taya wakati Simba ilipomenyana na Wydad Casablanca ya Morocco katika mechi ya raundi ya tatu ya michuano ya klabu bingwa Afrika, iliyochezwa wiki iliyopita mjini Cairo, Misri.
Kwa mujibu wa Basena, uongozi uliamua kuweka kambi mjini Tanga kwa vile kuna utulivu na wachezaji wangeweza kuelekeza zaidi akili zao katika mchezo wa Jumapili.
Tangu ilipoanza kambi mjini hapa, Simba imecheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya Kombaini ya mkoa wa Tanga na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1. Mechi hiyo ilichezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Basena alisema japokuwa hatambui vyema uwezo wa wapinzani wao, lakini amejifunza mengi kupitia mechi yao dhidi ya Waydad Casablanca na pia kurekebisha kasoro zilizojitokeza katika mchezo huo.
Wakati huo huo, mshambuliaji Emmanuel Okwi wa Simba amejiunga na kambi ya timu hiyo mjini Tanga kwa ajili ya maandalizi ya mechi yao dhidi ya DC Motema Pembe.
Okwi hakuwepo kambini kwa vile aliitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Uganda, ambacho mwishoni mwa wiki iliyopita, kilicheza mechi ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika za 2012.
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alisema jana kuwa, Okwi aliripoti kambini Jumatatu akiwa fiti na mwenye ari kubwa ya kuitumikia timu yake.
Kaburu alisema pia kuwa, kiungo Hillary Echessa naye amejiunga na kambi ya timu hiyo kwa ajili ya maandalizi ya mchezo, sanjari na wachezaji waliokuwemo kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars.
Kwa mujibu wa Kaburu, kikosi cha Simba kilirejea mjini Dar es Salaam jana kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kabla ya kuivaa Motema Pembe.
Kiongozi huyo wa Simba alisema, kipa Kaseja ameshaanza mazoezi mepesi na anatarajiwa kuwa fiti kabla ya mchezo huo. Kaseja alienguliwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kutokana na kuwa majeruhi.
Wakati Simba ikijiandaa kukabiliana na wapinzani wao hao, kuna habari kuwa, timu ya Motema Pembe inatarajiwa kuwasili nchini leo ikiwa na kikosi cha wachezaji 20.
Habari kutoka Congo zimeeleza kuwa, Motema Pembe iliamua kuhamishia kambi yake kutoka Goma hadi Kivu kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo.
Kwa sasa, Motema Pembe inanolewa na Kocha Andy Fulila baada ya kutimuliwa kwa Kocha Mohamed Nashridine Nabi kutokana na kushindwa kuwa na ushirikiano na wasaidizi wake.

No comments:

Post a Comment