KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 23, 2011

NITAIFUMUA TENA YANGA-TIMBE


SWALI: Kocha Sam Timbe, umerejea hivi karibuni kutoka mapumzikoni Uganda na tayari umeanza kuinoa Yanga kwa ajili ya msimu ujao. Mikakati yako ni ipi?
JIBU: Namshukuru Mungu nimepumzika vizuri hasa baada ya kuiwezesha Yanga kuibuka na ubingwa msimu uliopita. Ninachoweza kusema ni kwamba, kwa sasa nipo kwenye kipindi kigumu sana.
Unajua kuunda kikosi cha ushindi, inabidi utulie na kushirikiana na viongozi wa klabu pamoja na benchi la ufundi kuhakikisha mnakuwa na timu imara. Mkiweza kufanya hivyo, ndipo moyo unaweza kutulia.
Msimu ujao sisi tutakuwa tunawakilisha nchi kwenye michuano ya klabu bingwa Afrika, hivyo nikifanya usajili mbovu, lazima nitakuwa na kikosi bomu.
Nimeanza utaratibu wa kupima uwezo wa wachezaji wangu katika mazoezi na mechi tulizocheza hadi sasa kabla ya kuidhinisha rasmi usajili wao kwa ajili ya msimu ujao.
Nimewaangalia baadhi ya wachezaji wanaoitwa nyota kwenye mazoezi na mechi tulizocheza na kugundua kwamba, bado kuna wachezaji, ambao wanatakiwa kufanyakazi ya ziada ili waweze kufikia viwango ninavyovihitaji.
SWALI: Ni kipi hasa ulichokigundua kwa wachezaji hao hadi sasa na ni akina nani?
JIBU: Zipo kasoro kadhaa kwa baadhi ya wachezaji. Unajua mchezaji anapohama kutoka timu moja kwenda nyingine, atakumbana na wakati mgumu kwa vile atakutana na watu, ambao hajawazoea. Hivyo nitalazimika kufanya marekebisho kadhaa katika dosari nilizozibaini.
Tayari nimeshawaona baadhi ya wachezaji, ambao nimebaini kuwa uwezo wao ni mdogo. Nitakachokifanya ni kuwaongezea makali. Kama watashindwa kwenda na kasi ninayoihitaji, itabidi tuachane nao.
Kama unavyofahamu, kikosi changu kitashiriki michuano ya klabu bingwa. Huko tutakutana na timu bora kutoka kila nchi. Hivyo lazima nijenge timu imara na yenye kuweza kutoa ushindani. Hatutaki tushiriki michuano hiyo kama wasindikizaji.
Nawapongeza viongozi wa Yanga, hasa kamati ya usajili kwa kuweza kuyafanyiakazi mapendekezo niliyoyatoa kuhusu usajili wa wachezaji wapya. Kazi waliyoifanya kwa kweli ni nzuri sana na imefanywa kwa umakini mkubwa.
SWALI:Umesema kwamba bado hujaamua kikosi chako cha kwanza kitakavyokuwa. Una maana kwamba wapo baadhi ya wachezaji ambao utalazimika kuwaacha baada ya kusajiliwa na kamati?
JIBU: Ukweni ni kwamba bado Yanga hatujatangaza rasmi kikosi chetu cha msimu ujao. Lakini napenda nikueleze kwamba, mabadiliko lazima yatakuwepo.
Kuna baadhi ya wachezaji wa nje wanaweza kuongezwa. Nimepata taarifa kwamba baadhi ya klabu, ikiwemo Yanga, zimeomba idadi ya wachezaji wa kigeni iongezwe.
Idadi ya sasa ya wachezaji watano wa kigeni kutoka nje kwa kweli ni ndogo sana. Inabidi kocha awe makini kwa vile unaweza kusajili wachezaji wenye uwezo mdogo ikawa matatizo.
SWALI: Yanga imeruhusiwa kushiriki katika michuano ya mwaka huu ya Kombe la Kagame. Umejiandaa vipi na kikosi chako?
JIBU: Nimejiandaa vizuri na kupitia michuano hiyo natarajia nitaweza kupata kikosi cha kwanza kwa ajili ya michuano ya ligi kuu msimu ujao na ile ya klabu bingwa Afrika.
Pamoja na malengo hayo, nimeshaangalia uwezo wa wachezaji waliopo katika kikosi changu kupitia mazoezi na mchezo wetu wa kirafiki dhidi ya kombaini ya Ilala na nitaendelea kufanyakazi hiyo huko Arusha, ambako tunatarajia kucheza na Gor Mahia.
Jambo la msingi ni kwamba nimepanga kuitumia michuano hiyo kutafuta kikosi cha kwanza cha ligi kuu na michuano ya kimataifa.
SWALI: Umeuonaje mfumo wa uendeshaji wa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara?
JIBU: Binafsi nauona mfumo siyo mbaya, lakini yapo matatizo madogo madogo, likiwemo ratiba kuingiliana na michuano ya kimataifa, jambo ambalo linasababisha baadhi ya wachezaji kushindwa kuzitumikia klabu zao vizuri, hasa inapotokea wameitwa kwenye timu ya taifa.
Tatizo lingine nililolibaini ni kwamba, baadhi ya waamuzi wanashindwa kuzitafsiri vyema sheria 17 za soka na kusababisha wakati mwingine kuwepo na malalamiko kutoka kwa baadhi ya timu.
SWALI:Je, umepata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa viongozi wa klabu ya Yanga katika zoezi hili la usajili?


JIBU: Kwa kweli nawashukuru sana viongozi wa Yanga, hadi sasa tunakwenda vizuri, hakuna matatizo na hii ndiyo siri ya mafanikio ya kutwaa ubingwa msimu uliopita.

No comments:

Post a Comment