'
Thursday, June 9, 2011
Athumani Kambi, nyota mpya ya Sikinde
NI siku ya Jumamosi. Muda ni saa moja za usiku. Nipo kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam, ambako bendi ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra inatumbuiza.
Wakati nikiingia ukumbini, bendi hiyo ilikuwa ikiporomosha kibao kinachoitwa ‘Mume wangu Jerry’, kilichoimbwa na Hassan Bitchuka huku ukumbi ukiwa umesheheni mashabiki kedekede.
Macho yangu yakaelekea moja kwa moja stejini, ambako nilitegemea kumuona Bitchuka akiwa anaimba kibao hicho, lakini hakuwepo. Aliyeshika kipaza sauti alikuwa mtu mwingine tofauti. Nikashangaa.
Sauti ya kijana huyo haikuwa na tofauti hata chembe na ile ya Bitchuka. Hata mashabiki waliokuwepo ukumbini walionekana kumshangaa. Baadhi yao walihamasika kusogea karibu na steji ili kumshuhudia kwa karibu na pia kumshangilia.
Kijana huyo hakuwa mwingine zaidi ya Athumani Kambi, mwimbaji wa zamani wa bendi ya Vijana Jazz, ambaye pia aliwahi kupitia bendi za Sensema Malunde ya Tabora, Msondo Ngoma na Bwagamoyo Sound.
Mara baada ya kumaliza kuimba wimbo huo, mmoja wa waimbaji wa bendi hiyo, Abdalla Hemba alimtambulisha rasmi Kambi kwa mashabiki.
Hemba pia alitumia fursa hiyo kuwauliza mashabiki iwapo Kambi anafaa kujiunga na bendi hiyo au la. Kwa pamoja, mashabiki wengi waliitikia kwa sauti za juu kwamba anafaa kupewa nafasi hiyo.
Kwa mujibu wa Hemba, lengo la bendi yake ni kuziba mapengo ya waimbaji wa zamani na pia kuajiri vijana wenye damu changa kwa lengo la kuwaendeleza zaidi kimuziki.
Alisema walitumia muda mfupi kumjaribu Kambi kwa kumpa nafasi ya kuimba nyimbo mbalimbali za zamani za bendi hiyo, hasa zilizoimbwa na Bitchuka, Hussein Jumbe, Benovila Anthony na wengineo na aliweza kuzimudu barabara.
Hivyo ndivyo Kambi alivyoanza kuitumikia rasmi Mlimani Park Orchestra na tangu wakati huo, amekuwa mmoja wa wanamuziki kivutio kwa mashabiki kila bendi hiyo inapofanya maonyesho kwenye kumbi za DDC Kariakoo na klabu ya Sigara, Chang’ombe, Dar es Salaam.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam wiki hii, Kambi alisema ameamua kujiunga na Mlimani Park kwa lengo la kujiendeleza zaidi kimuziki na pia kubadili hali ya hewa.
“Unajua mwanamuziki ni mtu anayetembea sana na Sikinde inapiga muziki wa kiwango cha juu, hivyo lengo langu kubwa ni kujiendeleza zaidi kimuziki,”alisema.
“Muziki wa Sikinde ni wa kiufundi zaidi ndio sababu siyo wanamuziki wote wanaoweza kupigia bendi hii. Lakini kwa hatua niliyofikia sasa, nina uwezo wa kuimbia hata Twanga Pepeta, FM Academia na bendi zingine bila matatizo yoyote,”aliongeza.
Kambi alisema uundaji wa muziki katika bendi hiyo ni mgumu na unafanywa kwa utaalamu wa hali ya juu, hivyo kwake hiyo ni sehemu ya mafunzo zaidi ya kimuziki.
Tayari Kambi ameshashiriki kuimba vibao vitatu vipya vya bendi hiyo, vilivyotambulishwa rasmi Jumapili iliyopita kwenye viwanja vya klabu ya Sigara. Vibao hivyo ni Jinamizi la talaka, Nitalipa deni lako na Matatizo ya maisha.
Matarajio makubwa ya Kambi ni kuwa mwanamuziki wa kiwango cha juu zaidi na pia kupata mafanikio akiwa ndani ya Sikinde. Pia ametoa mwito kwa wanamuziki chipukizi kupenda kujifunza zaidi na kutokata tamaa mapema.
“Mwanamuziki hupaswi kukata tamaa mapema ama kuogopa kwenda bendi nyingine. Waache woga na wajitokeze zaidi,”alisema.
“Wazee wetu kama vile Bitchuka, wanakaribia kustaafu na wanahitaji warithi wao. Baadhi ya watu walinishangaa waliposikia nimeamua kwenda Sikinde, wakaniuliza utaweza kweli? Tuache woga, tuonyeshe vipaji vyetu, ukiwa na dosari utaelekezwa na huko ndiko kujifunza,”alisema.
Kambi alianza kuvutiwa na muziki tangu akiwa mdogo, ambapo alikuwa na uwezo wa kuimba nyimbo za wanamuziki mbalimbali wakongwe kama vile Shida na Georgina, zilizoimbwa na marehemu Mbaraka Mwinshehe na marehemu Marijani Rajabu.
Vilevile alikuwa akivutiwa na uimbaji wa wanamuziki wakongwe kama vile Bitchuka, marehemu Hemed Maneti, marehemu Nico Zengekala, Benovilla Anthony na wengineo.
Bendi yake ya kwanza ilikuwa Sensema Malunde yenye maskani yake mjini Tabora, inayoongozwa na mkongwe Madaraka Moris. Baadaye alipitia kwa muda mfupi Msondo Ngoma kabla ya kutua Bwagamoyo Sound.
Akiwa Vijana Jazz, Kambi alishiriki kuimba nyimbo zote zilizomo kwenye albamu ya mwisho ya bendi hiyo, inayojulikana kwa jina la ‘Misele’. Baadhi ya nyimbo hizo ni ‘Fanya mambo’, ‘Usingizi’ na ‘Tuepuke vishawishi’.
Mwanamuziki huyo ni mwenyeji wa mkoa wa Pwani na alisoma shule ya msingi, sekondari na kukulia katika mkoa huo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment