'
Thursday, June 23, 2011
VILLAS-BOAS ATUA RASMI CHELSEA
LONDON, England
HATIMAYE klabu ya Chelsea ya England imetangaza rasmi kumnyakua Kocha Andre Villas-Boas baada ya kukamilisha malipo ya kuvunja mkataba wake.
Chelsea imemnyakua kocha huyo mwenye umri mdogo kuliko makocha wa ligi kuu ya England, kutoka klabu ya FC Porto ya Ureno.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Chelsea jana ilieleza kuwa, klabu hiyo imeilipa FC Porto kitita cha pauni milioni 13.2 za Uingereza (sh. bilioni 29) kwa ajili ya kuvunja mkataba wake.
Kwa mujibu wa taarifa hayo, malipo hayo yalifanyika juzi usiku, ikiwa ni siku chache baada ya kuripotiwa kuwa, kocha huyo amewasilisha maombi ya kuvunja mkataba wake na FC Porto.
Kwa sasa, Villas-Boas yupo mapumzikoni, lakini huenda akaungana na baadhi ya maofisa wa Chelsea kwa ajili ya kukamilisha taratibu za uhamisho wake.
Habari kutoka ndani ya Chelsea zimeeleza kuwa, kocha huyo huenda akatambulishwa rasmi kwa waandishi wa habari mwezi ujao baada ya kuongoza mazoezi ya timu hiyo kwa siku chache.
Porto ilimtangaza rasmi kocha msaidizi wa timu hiyo, Vitor Pereira kuchukua nafasi ya Villas-Boas na pia kutoa taarifa kwa soko la hisa kwamba mkataba wa kocha huyo wa zamani umesitishwa.
Villas-Boas, ambaye alikuwa kufanyakazi Chelsea, akiwa msaidizi wa kocha wa zamani, Jose Mourinho, anatarajiwa kusajili wachezaji wawili wapya kutoka FC Porto. Wachezaji hao ni Falcao na Joao Moutinho.
Mbali na kusajili nyota hao wa FC Porto, kocha huyo pia anatarajiwa kuwasili London akiwa na wasaidizi wake wawili, akiwemo kocha wa viungo, Jose Maria Rocha na Daniel Souza.
Rais wa FC Porto, Jorge Nuno Pinto da Costa ametangaza rasmi thamani za wachezaji hao wawili kuwa ni pauni milioni 26.5 kwa Falcao na pauni milioni 35.5 kwa Moutinho.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment