MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Amani Temba amesema muziki anaoupiga si wa kihuni na kwamba umelenga kufundisha maadili mema kwa jamii.
Temba alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, nyimbo zake ndizo zinazoongoza kwa kutoa mafunzo yenye mwelekeo wa kuielimisha jamii.
Kiongozi huyo wa kundi la TMK Wanaume Family, alielezea msimamo wake huo baada ya kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wadau wa muziki huo kwamba, nyimbo zake nyingi zinapotosha jamii.
“Si kwamba najitetea, lakini kiukweli ni kwamba muziki wangu sio wa kihuni kama watu wanavyosema, unaongoza kwa kurekebisha jamii, huwezi kuamini,”alisema msanii huyo.
Temba ni mmoja wa wasanii wanaong’ara katika kundi la TMK, ambapo amekuwa akipenda kurekodi nyimbo zake binafsi kwa kushirikiana na Chege Chigunda.
Msanii huyo aliyezaliwa mwaka 1980, ambaye pia ni mchezaji mzuri wa mpira wa kikapu, amewahi pia kurekodi na wasanii wengine nyota kama vile Ray C, Dully Sykes na wengineo.
Kabla ya kujiunga na TMK, Temba alikuwa mmoja wa wasanii waliokuwa wakiunda kundi la Manduli Mobb pamoja na Juma Nature. Moja ya nyimbo zilizolipatia umaarufu kundi hilo ni ‘Maskini jeuri’ waliyoirekodi mwaka 2000.
Baadaye kundi hilo liligawanyika na kila msanii akaamua kufanyakazi kivyake. Wimbo wa kwanza wa Temba baada ya kujiengua katika kundi hilo unajulikana kwa jina la ‘Nakumindi’, aliourekodi mwishoni mwa 2001.
Msanii huyo baadaye alijiunga na kundi la TMK, ambapo aliibuka na kibao chake kilichompatia umaarufu, kinachokwenda kwa jina la ‘Nampenda yeye’. Alirekodi kibao hicho kwa kushirikiana na Dully Sykes.
No comments:
Post a Comment