KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, June 15, 2012

Kapombe mwanamichezo bora wa TASWA 2011

Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Ali Hassan Mwinyi akimkabidhi mwanamichezo bora wa mwaka 2011, Shomari Kapombe wa Simba tuzo yake baada ya kumtangaza kuwa mshindi katika sherehe zilizofanyika jana usiku kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.


Mchezaji wa zamani wa timu ya Coast Union ya Tanga na Timu ya Taifa Stars, Salim Amir akikabidhi tuzo ya mwanamichezo bora chipukizi kwa mchezaji Shomari Kapombe wa Simba.

Kapombe Mwanamichezo bora wa mwaka 2011, Shomari Kapombe akiwa ameshikilia mfano wa hundi ya sh. milioni 12 pamoja na Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Geofrey Nyange Kaburu, Mkurugenzi Mtendaji wa Serengeti, Richard Wells na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa kampuni hiyo, Teddy Mapunda.



Mwanasoka bora kwa wanawake, Mwanahamisi Omary 'Gaucho' akipokea tuzo yake kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Tanzania.


BEKI nyota wa klabu ya Simba na timu ya Taifa, Taifa Stars, Shomari Kapombe juzi usiku aliangua kilio ukumbini, baada ya kutangazwa kuwa mwanamichezo bora wa Tanzania kwa mwaka 2011.
Tukio hilo lilitokea wakati wa sherehe za utoaji wa tuzo kwa wanamichezo bora wa mwaka 2011 zilizoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) na kufanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Mara baada ya Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi kumtangaza kuwa ndiye mwanamichezo bora, Kapombe aliinamisha uso wake kwenye meza aliyokuwa amekaa na kuanza kutokwa machozi.
Ilibidi baadhi ya wachezaji wenzake wa Taifa Stars pamoja na Meneja wa timu hiyo, Leopard Tasso na Kocha Mkuu, Kim Poulsen wambembeleze na kumsindikiza stejini kupokea tuzo yake.
Baada ya kupokea tuzo hiyo kutoka kwa Mzee Mwinyi pamoja na pesa taslimu sh. milioni 12 na pia kupiga picha na viongozi mbalimbali, mchezaji huyo chipukizi alishindwa kujizuia kulia wakati alipokuwa akishuka stejini.
Kilichozidisha kilio chake ni kuwaona waandishi wa habari wakiwa wamemzunguka wakitaka kupata kauli yake kuhusu ushindi wake huo wa kihistoria. Kapombe alionekana kupatwa na kigugumizi, asijue nini la kuzungumza. Baadaye alitamka maneno machache akimshukuru Mungu kwa kupata tuzo hiyo pamoja na waandaaji kwa kumteua kuwa mshindi.
Alipotakiwa kuwataja watu waliochangia mafanikio yake, nyota huyo hakusita kutaja jina la kiungo wa zamani wa Simba, marehemu Patrick Mafisango, aliyefariki kwa ajali ya gari mwezi uliopita. Baada ya kutaja jina hilo, alizidisha kilio kabla ya wachezaji wenzake kuondoka naye.
Kabla ya kupewa tuzo hiyo, Kapombe pia alitangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya mwanamichezo chipukizi na kuzawadiwa pesa taslimu sh. milioni moja.
Tuzo ya heshima ilinyakuliwa na wachezaji wa zamani wa Taifa Stars waliokuwemo kwenye kikosi kilichofuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwaka 1979 baada ya kuitoa Zambia kwa mabao 2-1.
Baadhi ya wanasoka hao, ambao walizawadiwa sh. 200,000 kila mmoja ni Juma Pondamali, Daudi Salum, Salim Amir, Leodegar Tenga, Omari Hussein, Mohamed Rishard Adolph na Peter Tino. Tuzo za wachezaji, ambao wameshafariki dunia, zilipokewa na wake ama watoto wao.
Wanamichezo wengine walioshinda tuzo, michezo wanayocheza ikiwa kwenye mabano ni Mbwana Samatta (mwanamichezo bora anayecheza nje), Emmanuel Okwi (mwanamichezo bora wa nje), Mwanahamisi Omari (soka ya wanawake), Aggrey Morris (soka wanaume), Zakia Mrisho (riadha wanawake) na Alphonce Felix (riadha wanaume).
Wengine ni George Tarimo (kikapu wanaume), Evodia Kazinja (kikapu wanawake), Lilian Sylidion (netiboli), Madina Iddi (gofu wanawake), Frank Roman (gofu wanaume), Selemani Kidunda (ngumi za ridhaa), Magdalena Moshi (kuogelea wanawake), Ammar Ghadiyali (kuogelea wanaume).
Wanamichezo wengine ni Azzan Hussein (judo-Z’bar), Mbarouk Selemani (judo bara), Theresia Abwao (wavu wanawake), Mbwana Ally (wavu wanaume), Nasibu Ramadhani (ngumi za kulipwa), Waziri Salumu (tenisi wanaume), Rehema Athumani (tenisi wanawake), Sophia Hussein (baiskeli wanawake), Richard Laizer (baiskeli wanaume).
Wengine ni Kazad Monga (mikono wanaume), Zakia Seif (mikono wanawake), Monica Pascal (kriketi wanawake), Kassimu Nassoro (kriketi wanaume), Ahmada Bakar (olimpiki maalum Z’bar), Herith Suleiman (olimpiki maalum Bara), Zaharani Mwenemti (paralimpiki wanaume) na Faudhia Chafumbwe (paralimpiki wanawake).

No comments:

Post a Comment