RAIS Jakaya Kikwete jana aliendelea na utaratibu wake wa kukutana na viongozi wa vyama mbalimbali vya michezo baada ya kuwakaribisha Ikulu viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF).
Viongozi wa TBF waliofika Ikulu ni pamoja na Rais wa shirikisho hilo, Musa Mziya, Makamu wa Rais, Phares Magesa, Katibu Msaidizi, Michael Maluwe na Mhazini, Marry Mbaga. Pia alikuwepo Mkurugenzi Msaidizi wa Michezo kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Charles Matoke.
Katika kikao hicho, Magesa kwa niaba ya TBF alimweleza Rais Kikwete kuhusu maendeleo ya mchezo huo na hatua walizozichukua katika kuleta maendeleo.
Magesa pia alimkabidhi Rais Kikwete jezi ya timu ya New York Knicks yenye jina lake, ambayo ilitolewa na Kocha Greg Brittenham, aliyekuwepo nchini kwa ajili ya kuendesha mafunzo ya mchezo huo kwa vijana wa chini ya miaka 17.
Mafunzo hayo yalifanyika mkoani Arusha Juni 9-10 mwaka huu na yaliwashirikisha vijana 100 kati ya hao, 30 wakiwa wa kike na 70 wa kiume.
Makamu Mwenyekiti huyo wa TBF pia alimkabidhi Rais Kikwete jaketi maalumu la viongozi wa michezo kutoka Chuo Kikuu cha Wake Forest, ambacho Kocha Greg kwa sasa ni mkurugenzi wake wa michezo.
Kabla ya kujiunga na chuo hicho, Greg alikuwa kocha msaidizi wa New York Knicks kwa miaka 20 na ni mmoja wa makocha bora wa daraja la juu duniani katika mchezo huo.
Rais Kikwete aliishukuru TBF, Kocha Greg, timu ya New York Knicks na Chuo Kikuu cha Wake Forest kwa kumzawadia vifaa hivyo vya michezo.
Hii ni mara ya pili kwa Rais Kikwete kuwakaribisha viongozi wa vyama vya michezo Ikulu. Mwanzoni mwa wiki hii, Rais Kikwete aliwakaribisha na kuzungumza na viongozi wa Chama cha Riadha nchini (RT).
No comments:
Post a Comment