KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, June 20, 2012

Viongozi vyama vya michezo waache ubabaishaji tuzo za TASWA

Rais mstaafu wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi akimkabidhi tuzo ya mwanamichezo bora, mchezaji Shomari Kapombe wa Simba

Mwanahamisi Omari 'Gaucho' akipokea tuzo ya mwanasoka bora wa kike

Aggrey Morris akipokea tuzo yake ya mwanasoka bora wa mwaka 2012


Kwa miaka miwili mfululizo, nilikuwa mmoja wa wajumbe wa kamati ya tuzo za wanamichezo bora iliyoundwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA).
Kazi ya kamati hiyo, iliyoundwa na kamati ya utendaji ya TASWA mwaka jana, ilikuwa ni kusimamia mchakato wa kuwapata wanamichezo bora kwa kila chama na hatimaye mwanamichezo wa jumla.
Kamati hiyo chini ya mwenyekiti wake, mwanahabari mkongwe wa michezo nchini, Masoud Saanani, haikuwa na kazi ngumu katika kuwachagua wanamichezo bora. Ilikuwa ikipata ushirikiano mzuri kutoka kwa viongozi wa vyama vya michezo katika kutoa mapendekezo na sifa za wanamichezo wanaofaa kuwania tuzo hizo.
Kazi ya kamati hiyo haikuwa kupanga fedha za udhamini zitakavyotumika. Kazi hiyo ilikuwa ikifanywa na wadhamini, Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) kwa kushirikiana na TASWA.
Kamati ilijikita zaidi katika uteuzi wa wanamichezo bora kwa kuzingatia sifa zao katika ushiriki wa michuano ya ndani na kimataifa. Pia kamati ndiyo iliyobeba jukumu la kuteua watu wanaostahili kupewa tuzo ya heshima kutokana na mambo makubwa waliyoyafanya katika nchi hii.
Hata hivyo, inasikitisha kuona kuwa, baadhi ya vyama vya michezo havikuwa makini katika uteuzi wa wanamichezo wanaofaa kuwania tuzo hizo. Baadhi ya viongozi wa vyama waliweka mbele zaidi uswahiba na ukaribu kati yao na wanamichezo badala ya kuzingatia sifa zinazotakiwa.
Mbaya zaidi, kwa mwaka wa pili mfululizo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilishindwa kuwasilisha majina ya wanamichezo wake wanaostahili kuwania tuzo hiyo ili wapigiwe kura na kamati. Kazi hiyo ilifanywa na kamati kwa kuzingatia ushiriki wa wanasoka katika michuano ya ligi kuu na ya kimataifa.
Vyama vingine kama vile, Chama cha Riadha (RT) na Shirikisho la Mpira wa Kikapu (BFT) uteuzi wake ulikuwa unatia kichefuchefu kwa sababu wanamichezo walioteuliwa kuwania tuzo za michezo hiyo hawakuwa na sifa zinazotakiwa. Uteuzi wao ulifanywa kirafiki zaidi kuliko kuangalia ushiriki wa wachezaji katika michuano ya ndani na nje ya nchi.
Kwa mfano, majina ya wanariadha yaliyowasilishwa na RT kwa kamati yalikuwa mawili badala ya matatu na uteuzi ulifanywa na katibu mkuu wake, Suleiman Nyambui bila kuishirikisha kamati ya utendaji ama ua ufundi. Ni dhahiri kwamba uteuzi wa aina hii ni wa kibinafsi zaidi na hauwezi kuleta changamoto kwa vijana kupenda michezo.
Hali hiyo pia ilijitokeza katika uteuzi wa wachezaji wa mpira wa kikapu, ambapo wachezaji wawili walioteuliwa na BFT kuwania tuzo hiyo hawakuwa na sifa zinazotakiwa. Mwanamichezo ambaye alistahili tuzo hiyo, jina lake liliachwa kabisa. Ilibidi kamati itumie uzoefu wa wajumbe wake kutafuta mshindi wa tuzo ya kikapu.
Tatizo hilo pia lilijitokeza kwa Chama cha Netiboli nchini (CHANETA). Badala ya kuwasilisha majina ya wachezaji wake watatu wanaostahili kuwania tuzo hiyo, kiliwasilisha majina ya wachezaji wawili huku jina moja likiwa na sifa nzuri zaidi kuliko lingine. Hii inamaanisha kwamba, chama hicho kilishakuwa na pendekezo lake mapema.
Utata mwingine ulizuka katika mchezo wa ngumi za kulipwa, ambao hadi sasa haieleweki upo chini ya chama kipi. Karibu kila chama kiliwasilisha jina la mabondia wake. Kulikuwa na vyama vilivyojitambulisha kwa majina ya TPBO, PST na TPBF. Ilibidi kamati ipitie kwa umakini sifa za mabondia wote, ambao majina yao yaliwasilishwa na vyama hivyo kabla ya kufanya uteuzi wa bondia bora.
Baadhi ya vyama kama vile mpira wa magongo, judo, kriketi, tennis, gofu, kuogelea, mikono, wavu, olimpiki maalumu na paralimpiki vilifanya uteuzi mzuri na wa umakini. Mbali na kuwasilisha majina matatu, vilieleza kwa kirefu sifa za kila mchezaji nap engine kutoa mapendekezo yupi alistahili zaidi kuwa bora kutokana na sifa zake.
Navipongeza vyama vyote vilivyoonyesha umakini mkubwa katika uteuzi wake kwa sababu ulizingatia mambo yote muhimu yaliyoelekezwa na kamati kwa lengo la kuzifanya tuzo hizo ziwe na heshima zaidi.
Kwa vyama vilivyovurunda kama vile BFT, RT na TFF, ambayo imeshindwa kuwasilisha majina ya wanamichezo wake kwa mara ya pili mfululizo, navishauri viwe makini na viziheshimu tuzo hizi, ambazo kwa sasa zimeanza kujipatia umaarufu na heshima kubwa hapa nchini.
Kwa wanaokumbuka tuzo za mwaka jana, bila shaka wanayakumbuka maneno ya busara yaliyosemwa na mshindi wa tuzo ya heshima, Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa. Pia bila shaka wanakumbuka jinsi tuzo hizo zilivyopokelewa kwa mtazamo chanya na watanzania wengi.
Na bila shaka watanzania watazikumbuka nasaha zilizotolewa na Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi katika tuzo za mwaka huu na jinsi watanzania walivyofurahia kuona wanasoka wao wa zamani, walioiwezesha Taifa Stars kufuzu kucheza fainali za Afrika mwaka 1980 walivyoenziwa na kuthaminiwa.
Kwa kuwa tuzo hizi zitakuwa zikitolewa kila mwaka, nawashauri viongozi wa vyama vya michezo vilivyovurunda, waache ubabaishaji. Wafanye uteuzi wao kwa kuzingatia sifa za wanamichezo wao katika ushiriki wa mashindano ya ndani na nje ya nchi.
Kupendekeza majina ya wanamichezo bora kwa sababu ya uswahiba ama ukaribu kati yao na viongozi ni kuwakatisha tamaa wanamichezo wengine na pia kufifisha juhudi zao katika kupeperusha vyema bendera ya Tanzania kimataifa.
Pengine kikubwa zaidi ni kwa wadhamini, SBL kuweka wazi kwa TASWA ripoti ya matumizi ya fedha za udhamini, badala ya ilivyo sasa, ambapo kazi zote kama vile uteuzi wa ukumbi, kuulipia, uandaaji wa vyakula na vinywaji, burudani na nyinginezo zimekuwa zikifanywa na maofisa wa kampuni hiyo.
Hali hiyo imekuwa ikiwafanya viongozi wa TASWA wajione wanyonge na pia kutumiwa kama mwamvuli na maofisa wa SBL, ambao wamekuwa wakijilimbikizia kazi zote kama vile chama hicho hakina uwezo wa kufanya yote hayo.

No comments:

Post a Comment