KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, June 20, 2012

Wema ampandia dau Omotola

Wema Sepetu

Omotola Jalade


MWIGIZAJI nyota wa filamu, Wema Sepetu amemwalika nchini msanii nguli wa fani hiyo kutoka Nigeria, Omotola Jalade Ekeinde.
Wema, ambaye ni mshindi wa taji la Miss Tanzania mwaka 2006, ameamua kumleta Omotola kwa ajili ya kupamba uzinduzi wa filamu yake mpya inayojulikana kwa jina la Super Star, itakayozinduliwa Jumamosi.
Filamu ya Super Star inazungumzia maisha ya Wema tangu alipokuwa mtoto na pia kushiriki kwake katika mashindano ya Miss Dar Indian Ocean, Miss Kinondoni na Miss Tanzania hadi kujitosa kwake katika uigizaji.
Wema amecheza filamu hiyo kwa kushirikiana na baadhi ya waigizaji nyota nchini kama vile Jacob Steven (JB), Hemed Mlela na wasanii nyota wa muziki wa kizazi kipya, Khaleed Mohamed (TID), Mr Blue, Judith Wambura (JayDee) na Barnaba.
Mrembo huyo wa zamani wa Tanzania ametumia zaidi ya sh. milioni 29 kwa ajili ya kutengeneza filamu hiyo ya kwanza kwake tangu alipoanza kuwa mtayarishaji na muongozaji wa filamu.
Akizungumza kwa njia ya simu juzi, Wema alithibitisha kufanya mipango ya kumleta Omotola na kuongeza kuwa, taarifa zaidi kuhusu ujio wa nyota huyo wa Nollywood zitatolewa baadaye.
Kwa mujibu wa Wema, nyota huyo wa Nigeria anatarajiwa kutua nchini wiki hii kwa ajili ya uzinduzi wa filamu hiyo, uliopangwa kufanyika wikiendi hii.
Omotola ndiye mwigizaji ghali wa kike nchini Nigeria, akiwapiku waigizaji wenzake, Ini Edo na Genevieve Nnaji. Mbali na uigizaji, Omotola pia ni mwanamuziki.
Kabla ya Omotola kupanda chati, Ini Edo na Genevieve waliwahi kushika namba moja kwa utajiri kwa nyakati tofauti miongoni mwa waigizaji wa kike nchini Nigeria.
Omotola alianza kutamba kwenye tasnia hiyo baada ya kutoka na filamu iitwayo Iva mwaka 1993. Hadi sasa nyota huyo ameshacheza filamu zaidi ya 52, zikiwemo, Ties That Bind (2011), A Private StormIje (2010), My Last Ambition (2009), Beyonce & Rihanna (2008), Temple of Justice (2008), Tomorrow Must Wait (2008) na nyinginezo kadhaa.

No comments:

Post a Comment