JAMHURI imewasilisha maombi Mahakama ya Rufani Tanzania, kuomba kupitia uamuzi wa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Dk. Fauz Twaib wa kukubali kufanyia uchunguzi wa umri wa msanii wa filamu Elizabeth Michael 'Lulu'.
Hati hiyo ya maombi ya Jamhuri iliwasilishwa jana Mahakama ya Rufani ikiiomba ipitie uamuzi wa Jaji Dk. Twaib alioutoa Juni 11, mwaka huu kwa madai kuwa, una makosa.
Juni 11, mwaka huu, Jaji Dk. Twaib, aliamua suala la uchunguzi wa umri wa Lulu, litasikilizwa Mahakama Kuu na kupatiwa ufumbuzi, licha ya maombi hayo ya msanii huyo, kuletwa kimakosa.
Wakili wa Serikali Elizabeth Kaganda, alidai hayo jana katika Mahakama Kuu, mbele ya Jaji Dk. Twaib, wakati maombi ya uchunguzi wa umri wa Lulu yalipotajwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.
Lulu anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya msanii mwenzake, Steven Kanumba iliyopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, anawakilishwa na mawakili Keneth Fungamtama akisaidiana na Flugence Massawe na Peter Kibatala.
Mawakili hao walidai kwamba wapo tayari kwa usikilizwaji wa maombi hayo. Katika maombi hayo, tayari mawakili wa Lulu na Jamhuri walishawasilisha ushahidi wao wa hati za viapo na wa maandishi ili kutatua juu ya umri wa muombaji huyo.
Hata hivyo, Wakili Elizabeth aliiomba Mahakama Kuu kuahirisha usikilizwaji wa maombi hayo kwa muda kwa kuwa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), imewasilisha hati ya Mahakama ya Rufani kuomba kupitiwa kwa uamuzi wa Jaji huyo kwa kuwa una makosa.
Ombi hilo la kuahirishwa kwa muda usikilizwaji wa maombi hayo lilipingwa na mawakili wa Lulu, Fungamtama na Kibatala kwa madai kwamba hakuna amri iliyotoka Mahakama ya Rufani ya kuahirishwa usikilizwaji huo.
Fungamtama alidai kuwa mahakama hiyo haiwezi kuahirisha usikilizwaji huo kutokana na maombi ya Jamhuri kwani ilipaswa iwepo amri kutoka Mahakama ya Rufani.
Pia alidai katika hati yao ya maombi, hakuna sehemu ambayo wanaomba ahirisho la usikilizwaji wa maombi hayo hadi hapo Mahakama ya Rufani itakapotoa uamuzi.
Wakili Fungamtama alidai kuwa kitendo cha DPP kuwasilisha hati hiyo jana ni kuharibu mwenendo wa mahakama.
Kwa upande wake, Wakili Kibatala alidai Jamhuri imechelewa kuwapa hati hiyo ya maombi ya kupitia uamuzi wa Jaji.
Akijibu hoja hizo, Wakili Elizabeth alidai wamewasilisha maombi hayo jana na kupewa namba na kwamba wao walipewa na Mahakama na hivyo kuamua kuwapatia mawakili hao kwani si kazi yao.
Wakili Elizabeth alikiri kwamba hakuna amri ya Mahakama ya Rufani iliyoletwa Mahakama Kuu ya kusimamishwa kwa usikilizwaji huo, alisikia ipo na itapelekwa hivyo kama haijafika suala hilo lipo nje ya uwezo wake.
Pia aliiomba mahakama kuahirisha usikilizwaji huo na kwamba wanaiachia itoe uamuzi wake wa kukubali au kukataa hivyo si kazi yao ni ya mahakama.Mbali na hilo, Wakili huyo alidai nia ya ofisi ya DPP ni kuona haki inatendeka.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Dk. Twaib aliamua kuwa amezingatia hoja hizo na ameiona hati hiyo ya maombi ya Jamhuri hivyo hawezi kupoteza muda wa kuendelea kusikiliza maombi hayo wakati muda wowote mwenendo wa kesi na uamuzi wake utaitwa Mahakama ya Rufani.
Jaji huyo alisema kuwa maombi hayo yataahirishwa kwa muda mfupi hadi Julai 9, mwaka huu yatakaposikilizwa.
Pia aliamuru kusimamishwa kwa mwenendo wa kesi katika Mahakama ya Kisutu, hadi hapo utakapotolewa uamuzi na Mahakama za juu kama alivyoamuru Juni 11, mwaka huu.
Jaji Dk. Fauz alitoa uamuzi wa kusimamishwa kwa mwenendo huo, baada ya Wakili wa Lulu, Fungamtama kuomba maelekezo ya mahakama kutokana na ofisi ya DPP na Mahakama ya Kisutu kufungua faili la dharura na kuendelea na mwenendo wakati ulisimamishwa.
Akiwasilisha hoja hiyo, Wakili Fungamtama alidai licha ya Mahakama Kuu kusimamisha mwenendo wa kesi ya mauaji inayomkabili Lulu, lakini bado mteja wao alifikishwa Mahakama ya Kisutu.
No comments:
Post a Comment