KOCHA Msaidizi wa timu ya soka ya Yanga, Fred Felix Minziro ameapa kuwa, lazima walipize kisasi cha kufungwa mabao 5-0 na watani wao wa jadi Simba katika mechi ya ligi kuu.
Akizungumza mjini Dar es Salaam juzi, Minziro alisema kipigo hicho kilikuwa cha kufedhehesha na bado kinaendelea kuisumbua akili yake hadi sasa.
Minziro alisema iwapo watakutana na Simba katika michuano yoyote, watafanya kila wanaloweza kushinda mechi hiyo na kupata ushindi mnono wa mabao.
Mchezaji huyo wa zamani wa Yanga alisema faraja pekee atakayoipata katika kazi yake hiyo ni kuiongoza timu yake kulipa kisasi hicho.
Kwa mujibu wa Minziro, Yanga inatarajiwa kuanza rasmi mazoezi wiki hii baada ya wachezaji wote kuripoti kambini kwa maandalizi ya michuano ya Kombe la Kagame.
Alisema mazoezi hayo yataanzia gym kwa ajili ya kuwaweka fiti wachezaji na baadaye kuhamia kwenye fukwe za bahari ili kuwaongezea stamina.
Yanga inaweza kukutana tena na Simba katika michuano ya Kombe la Kagame, inayotarajiwa kufanyika mwezi ujao mjini Dar es Salaam. Michuano hiyo pia itawashirikisha washindi wa pili wa ligi kuu, Azam.
Kipigo ilichokipata Yanga kutoka kwa Simba kilizua kizaazaa kikubwa kwa vijana hao wa Jangwani, ambapo viongozi wake kadhaa akiwemo mwenyekiti, Lloyd Nchunga walilazimika kujiuzulu.
Kujiuzulu kwa Nchunga na wajumbe wenzake wa kamati ya utendaji, kumeifanya klabu hiyo isiwe na uongozi unaotambulika kikatiba. Uchaguzi mkuu wa klabu hiyo umepangwa kufanyika Julai 15 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment