KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, June 20, 2012

Milovan kutua J'tatu

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Simba, Milovan Cirkovic anatarajiwa kutua nchini Juni 25 mwaka huu akitokea mapumzikoni nchini Serbia.
Milovan alikwenda Serbia kwa mapumziko mara baada ya kumalizika kwa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara, ambapo aliiongoza Simba kutwaa ubingwa.
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alithibitisha jana kuhusu tarehe ya kurejea kwa kocha huyo na kuongeza kuwa, anatarajiwa kuanza kazi mara moja.
Simba ilianza mazoezi wiki mbili zilizopita ikiwa chini ya Kocha Abdalla Kibadeni, ambapo kwa kuanzia, wachezaji walikuwa wakijifua kwenye gym.
Kaburu alisema Simba inatarajiwa kuondoka Dar es Salaam kesho kwa ndege kwenda Mwanza na Shinyanga kwa ziara ya mechi mbili za kirafiki dhidi ya Toto African na Express ya Uganda.
Mabingwa hao wa Tanzania Bara watacheza mechi ya kwanza keshokutwa kwa kumenyana na Toto African kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kabla ya kuvaana na Express siku inayofuata kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Katika hatua nyingine, beki mpya wa klabu ya Simba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo anatarajiwa kutua nchini leo.
Habari kutoka ndani ya Simba zimeeleza kuwa, beki huyo atasajiliwa kwa ajili ya kuziba pengo la Kelvin Yondan, aliyejiunga na klabu ya Yanga.
Kwa mujibu wa habari hizo, tayari beki huyo, ambaye jina lake linafanywa kuwa siri, ameshafanya mazungumzo ya awali na uongozi wa Simba na kukubaliana baadhi ya mambo.
Mbali na beki huyo, tayari Simba imeshamsajili kipa Hamadi Waziri kutoka JKT Oljoro kwa ajili ya kuziba pengo la Ally Mustapha ‘Barthez’ aliyehamia Yanga.
Simba pia imeamua kuwapandisha daraja wachezaji watatu kutoka kikosi chake cha pili. Wachezaji hao ni Jamal Mwambeleko, Omar Salum na William Lucian.

No comments:

Post a Comment