KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, June 27, 2012

MANJI AKATIWA RUFANI TFF

WAGOMBEA wawili wa uongozi katika uchaguzi mdogo wa klabu ya Yanga wamekatiwa rufani na baadhi ya wanachama kwa madai kuwa, hawana sifa zinazotakiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura aliwataja wagombea hao kuwa ni Yussuf Manji na Yono Kevela.
Katika uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Julai 15 mwaka huu, Manji anawania nafasi ya mwenyekiti wakati Kevela anawania nafasi ya makamu mwenyekiti.
Hata hivyo, Wambura hakutaja majina ya wanachama waliowakatia rufani wagombea.
Alisema mwanachama aliyemkatia rufani Manji, amewasilisha pingamizi 14 dhidi ya mgombea huyo wakati Kevela amekatiwa rufani moja.
Wambura alisema pia kuwa, baadhi ya wanachama wamekata rufani dhidi ya kamati ya uchaguzi ya klabu hiyo kwa madai ya kuwapitisha Manji na Kevela wakati hawana sifa za uongozi.
Kwa mujibu wa Wambura, rufani hizo zinatarajiwa kujadiliwa wiki ijayo katika kikao cha Kamati ya Uchaguzi ya TFF, inayoongozwa na Deo Lyattu.
Naye Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hamidu Mbwelezeni alisema jana kuwa, wamepanga kuzijadili rufani hizo wiki ijayo kwa vile Lyattu yupo nje ya nchi.
Hii ni mara ya pili kwa Manji kuwekewa pingamizi na wanachama wa Yanga kwa ajili ya uchaguzi huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa klabu hiyo.
Awali, mwanachama Ishashabaki Ruta alimwekea pingamizi Manji kwa kamati ya uchaguzi ya klabu hiyo kwa madai kuwa, hana sifa na amekuwa chanzo cha migogoro mingi ndani ya klabu hiyo.
Hata hivyo, pingamizi hilo lilitupwa baada ya kubainika kuwa Ishashabaki hakuwa mwanachama halali wa Yanga na alishindwa kwenda kutetea hoja zake siku ya kusikilizwa.
Akizungumza na Burudani jana kwa njia ya simu kuhusu rufani aliyokatiwa kwa kamati ya uchaguzi ya TFF, Manji aliwataka wanachama wa Yanga wawe na watulivu na wenye subira.
Manji alisema hana wasiwasi kuhusu rufani hiyo kwa vile inafanana na pingamizi alilowekewa awali na kutupwa na kamati ya uchaguzi ya Yanga.
“Nawaomba wana Yanga wasiwe na wasiwasi kwa sababu naamini haki itatendeka na uchaguzi wetu utafanyika kama ilivyopangwa,”alisema.
Uchaguzi mdogo wa Yanga umeitishwa baada ya kujiuzulu kwa mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Lloyd Nchunga, makamu wake, Davis Mosha na wajumbe wanne wa kamati ya utendaji.

No comments:

Post a Comment