MMOJA wa wanamuziki waasisi wa bendi ya muziki wa dansi ya Mapacha Watatu, Jose Mara amesema kujitoa kwa Kalala Junior hakutaiyumbisha bendi hiyo.
Jose alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, bendi yao bado ipo imara na hakuna kilichoharibika wala kitakayoifanya iyumbe na kutetereka.
“Wapo wanamuziki wengi ndani ya Mapacha Watatu, ambao ni wazuri na nina hakika tutafanya nao kazi kama ilivyokuwa kwa Kalala,”alisema.
“Ninachoweza kuwahakikishia mashabiki wetu ni kwamba kuanzia sasa tutapiga kazi ile mbaya kwa sababu hao vijana tutakaowaongeza ni wazuri kwa hiyo mambo yatakuwa mazuri, “alisema.
Jose aliwataka mashabiki wa bendi hiyo wasivunjike moyo bali waendelee kuwaonga mkono kwa vile wanamuziki waliopo ni wapambanaji.
Mwasisi mwingine wa bendi hiyo, Khalid Chokoraa alisema katika kudhihirisha kwamba bado wapo imara, wamerekodi singo mpya inayojulikana kwa jina la Ona Naonewa.
Kwa mujibu wa Chokoraa, wanatarajia kuitambulisha singo yao hiyo wakati wa maonyesho yao yatakayofanyika hivi karibuni mjini Dar es Salaam.
Kalala alitangaza kujitoa Mapacha Watatu hivi karibuni kwa madai kuwa, anataka kujipumzisha na masuala ya muziki.
Wakati huo huo, Meneja wa Mapacha Watatu, Hamisi Dacota amesema Kalala aliamua kuondoka kwenye bendi hiyo bila kukorofishana na wenzake.
Dacota alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, wanamtakia kila la heri Kalala katika mipango yake ya baadaye na milango ipo wazi iwapo atataka kurejea kwenye bendi hiyo.
“Kama mwanamuziki mwenzetu na kijana mwenzetu, tunamtakia kila heri huko aendako, lakini kama akitaka kurudi, milango iko wazi, anakaribishwa sana kwa sababu yeye ni mmoja wa waasisi wa bendi ya Mapacha Watatu," alisema Dacota.
No comments:
Post a Comment