WACHEZAJI wa timu ya soka ya vijana wa chini ya miaka 20 ya wilaya ya Mjini Magharibi wameahidiwa kitita cha sh. milioni 12 iwapo watatwaa ubingwa wa mashindano ya Rolling Stone.
Ahadi hiyo ilitolewa juzi na Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo, Said Ali Mbarouk na Rais wa ZFA, Amaan Makungu wakati walipokuwa wakiagana na wachezaji hao katika hafla iliyofanyika kwenye hoteli ya Bwawani mjini hapa.
Wakati Waziri Mbarouk aliwaahidi wachezaji hao kuwapatia sh. milioni saba iwapo watatwaa ubingwa, Makungu aliwaahidi kitita cha sh. milioni tano.
Mbarouk aliwataka wachezaji wa timu hiyo kuhakikisha wanafanya vizuri katika mashindano ya Rolling Stone kwa kurudo nyumbani na ubingwa badala ya kuwa washiriki.
Mashindano ya Rolling Stone, ambayo huzishirikisha timu za vijana kutoka nchi za ukanda wa Afrika Mashariki, yamepangwa kuanza Julai 7 mwaka huu mjini Bujumbura, Burundi.
Mbarouk aliwataka wachezaji hao kuzingatia maelekezo ya makocha na viongozi wao muda wote wa mashindano hayo na pia kuweka nidhamu mbele.
Alisema ushindi wa timu hiyo katika mashindano hayo utakuwa zawadi nzuri kwa rais mpya wa chama hicho, Makungu aliyechaguliwa kushika wadhifa huo mwishoni mwa wiki iliyopita.
Naye Makungu aliwataka vijana hao kuyatumia mashindano hayo kulitangaza vyema jina la Zanzibar kimataifa. Alisema iwapo watashika nafasi ya pili, atawazawadia kitita cha sh. milioni tatu.
No comments:
Post a Comment