KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, July 4, 2012

ATHUMANI IDDI CHUJI: SITAKI TENA UPUUZI

KIUNGO nyota wa klabu ya Yanga, Athumani Iddi ‘Chuji’ amesema amechoka kuendelea kujihusisha na mambo ya kipuuzi katika maisha yake na sasa ameamua kucheza soka.
Chuji amesema amepania kuendelea kucheza soka ya kiwango cha juu ili kumvutia Kocha Kim Poulsen amrejeshe kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars.
Mchezaji huyo wa zamani wa klabu ya Simba na Polisi Dodoma alisema hayo mwanzoni mwa wiki hii alipokuwa akizungumza na Burudani kuhusu mustakabali wake kisoka.
Chuji, ambaye makali yake yalianzia Polisi Dodoma kabla ya kusajiliwa na Simba na baadaye Yanga, alisema hataki tena kufanya mambo ya kipuuzi zaidi ya kuelekeza akili yake katika kucheza soka.
“Kama ni upuuzi, nimeufanya sana. Sasa nimeamua kucheza soka, mambo ya zamani naachana nayo kabisa, ‘ alisema kiungo huyo, ambaye pia ana uwezo wa kucheza nafasi ya beki wa kati.
‘Niliwahi kukumbwa na matatizo mengi nilipokuwa Simba na baadaye Yanga. Siwezi kurudia makosa. Nimeamua kubadili kabisa mfumo wangu wa maisha na soka,’ alisisitiza.
Chuji alisema katika kujiweka fiti, atahakikisha anaongeza bidii katika mazoezi na kujituma zaidi uwanjani ili kuhakikisha kiwango chake kinaendelea kuwa cha juu.
Alisema kushuka na kupanda kwa kiwango chake katika miaka ya hivi karibuni ni matokeo ya matatizo, ambayo aliwahi kukumbana nayo katika maisha yake na kumfanya aathilike kisaikolojia.
Hata hivyo, Chuji hakutaka kuweka wazi kuhusu matatizo hayo zaidi ya kusema ni vitu vya kawaida kutokea katika maisha ya mwanadamu.
‘Ninachoweza kusema kaka yangu, mambo ya kijinga nimeamua kuachana nayo kabisa, ‘ alisema.
Katika kudhihirisha dhamira yake hiyo, Chuji alisema ataongeza muda wa ziada wa kufanya mazoezi zaidi ya yale anayofanya na wachezaji wenzake akiwa na Yanga.
‘Kama sitakuwa na kipindi cha mazoezi na Yanga, nitakwenda kujifua mchangani. Nataka mwili wangu uwe fiti wakati wote, ‘ alisema kiungo huyo, ambaye aliwahi kutemwa kwenye kikosi cha Taifa Stars na Kocha Marcio Maximo kutoka Brazil kwa tuhuma za utovu wa nidhamu.
Chuji alisisitiza kuwa, bado ana dhamira ya dhati ya kurejeshwa tena kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa vile anaamini kuwa, uwezo wake kisoka upo juu.
Kiungo huyo, ambaye kwa sasa ni kivutio kikubwa kwa mashabiki wa Yanga kutokana na kucheza soka kwa kujiamini amedokeza kuwa, uongozi wa klabu hiyo umeamua kumuongezea mkataba wa mwaka mmoja.
Alisema alitia saini mkataba huo hivi karibuni na kuongeza kuwa, atahakikisha anaisaidia vyema Yanga katika michuano ya ligi na kimataifa.
‘ Siwadai chochote Yanga. Wao ndio wanaonidai mimi na sina budi kuwalipa kwa kuonyesha uwezo wangu uwanjani,’ alisema.
‘Na pia sitarajii kuondoka tena Yanga hivi karibuni na kwenda timu nyingine. Upo uwezekano mkubwa nitastaafu soka nikiwa Yanga,’ aliongeza.
Akizungumzia usajili wa wachezaji wapya uliofanywa na Yanga kwa ajili ya msimu ujao, Chuji alisema unatisha kwa vile wamesajiliwa vijana wengi wazuri na wenye damu changa.
Alisema kuwepo kwa damu changa kwenye kikosi cha Yanga kutaongeza chachu zaidi ya mafanikio kwa timu hiyo kwa vile wanacheza kwa kasi na kujituma muda wote wa mchezo.
Chuji pia aliupongeza uongozi wa Yanga kwa kumsajili beki Kelvin Yondan kutoka Simba, ambaye kutokana na uwezo wake, alisema atakuwa na msaada mkubwa kwa timu hiyo.
‘Kusema ule ukweli, kwa kumsajili Yondani, Yanga imelamba dume,’alisema.
‘Namfahamu vyema Yondan kwa sababu nimecheza naye nikiwa Simba na Taifa Stars. Ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa na anacheza kwa kujiamini na kujituma. Nitahakikisha nampa msaada wa kila aina ili aweze kufika mbali zaidi,’ aliongeza kiungo huyo.
Chuji alisema mara baada ya Yondan kujiunga na Yanga, alifanya naye mazungumzo kwa muda mrefu na amemuhakikishia kwamba, anataka kuipa heshima klabu hiyo.
Alisema naye amemweleza wazi Yondan kuwa anapaswa kuwa makini na kujiwekea malengo ya kufika mbali na kujiepusha na majungu na vitendo vinavyoweza kushusha kiwango chake.
‘Nimemweleza Yondan asisikilize majungu. Akili yake iwe kwenye soka tu na awe na malengo ya kucheza soka ya kulipwa badala ya kuishia hapa hapa Bongo, ‘alisema.

No comments:

Post a Comment