KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, January 8, 2016

SAMATTA ASHINDA TUZO YA MWANASOKA BORA WA AFRIKA KWA WACHEZAJI WA NDANI



MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora Anayecheza Afrika katika sherehe zilizofanyika usiku huu ukumbi wa mikutano wa Kimataifa mjini Abuja.
Samatta amepata pointi 127, mbele ya mchezaji mwenzake wa TP Mazembe, kipa Robert Muteba Kidiaba wa DRC, aliyepata pointi 88, wakati mshambuliaji wa Etoile du Sahel ya Tunisia na timu ya taifa ya Algeria, Baghdad Bounedjah amepata pointi 63.
Mafanikio ya Samatta anayeweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kushinda tuzo kubwa ya Afrika, yanakuja baada ya kuiwezesha Mazembe kutwaa taji la tano la Ligi ya Mabingwa Afrika, huku akiibuka mfungaji bora kwa mabao yake nane.
Mshambuliaji wa Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang ameshinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika kwa mara ya kwanza.
Mchezaji wa Borussia Dortmund ya Ujerumani mwenye umri wa miaka 26, amewaangusha Yaya Toure wa Ivory Coast aliyekuwa anashikilia tuzo hiyo na Andre Ayew wa Ghana.
Amekusanya pointi 143, saba zaidi ya Toure wakati Ayew ameshika nafasi ya tatu kwa kupata pointi 112 na anakuwa mchezaji wa kwanza wa
Gabon kushinda tuzo ya CAF
Kiungo wa Nigeria, Etebo Peter Oghenekaro ameshinda tuzo ya Mchezaji Anayechipukia Vizuri dhidi ya Mnigeria mwenzake, Azubuike Okechukwu, kipa wa Mali, Djigui Diarra, Mahmoud Abdelmonem Abdelhamid ‘Kahraba’ wa Misri na Mualgeria, Zinedine Ferhat.
Etebo, anayechezea timu ya Ligi Kuu ya Nigeria, Warri Wolves, aling’ara katika michuano ya U-23 ya Afrika Desemba nchini Senegal, akiibuka mfungaji bora kwa mabao yake matano, yakiwemo mawili aliyofunga katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Algeria katika fainali.
Mshambuliaji kinda wa Nigeria, Victor Osimhen ameshinda tuzo ya Mwanasoka Bora Chipukizi akimshinda ndugu yake, Kelechi Nwakali, wachezaji wawili wa Mali, Adama Traore na Samuel Diarra na Yaw Yeboah wa Ghana.
Osimhen anayeshinda tuzo hiyo siku tisa tangu asherehekee kufikisha miaka 17 ya kuzaliwa, mafanikio hayo yanafuatia kufanya kwake vizuri katika Kombe la Dunia la U-17 Oktoba mwaka jana nchini Chile, akifunga mabao 10 na kuibuka mfungaji bora sambamba na kushinda Mpira wa Fedha baada ya Mchezaji Bora wa pili wa michuano hiyo, huku Nigeria ikitwaa Kombe.
Anakuwa mchezaji wa pili wa Nigeria kushinda tuzo hiyo baada ya Kelechi Iheanacho mwaka jana.
Mfaransa, Herve Renard ameshinda tuzo ya kocha bora wa mwaka kwa mara ya pili, baada ya kuipa Ivory Coast ubingwa wa Afrika mwaka jana nchini Equatorial Guinea.
Mfaransa huyo amewashinda Baye Ba wa Mali U-17, Patrice Carteron wa TP Mazembe, Faouzi Benzarti wa Etoile du Sahel na Emmanuel Amunike wa Nigeria U-17
Renard, ambaye alishinda tuzo ya kwanza baada ya kuipa Zambia ubingwa wa Afrika mwaka 2012, alikabidhiwa tuzo yake na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF, Adoum Djibrine.
Cameroon imezishinda Ghana, Afrika Kusini na Zimbabwe katika kipengele cha timu bora ya taifa ya wanawake, wakati Ivory Coast imeziangusha
Ghana, Mali U-17, Nigeria U-17 na Nigeria U-23 katika timu bora ya taifa ya wanaume.
Refa wa Gambia, Papa Bakary Gassama ameshinda tuzo ya refa bora kwa mara ya pili mfululizo akiwaangusha Ghead Zaglol Grisha wa Misri, Janny Sikazwe wa Zambia na Eric Arnaud Otogo Castane wa Gabon.
Mualgeria, Haimoudi Djamel pia alishinda tuzo hiyo mara mbili mfululizo mwaka 2012 na 2013.

CHANZO CHA HABARI: BLOGU YA BINZUBEIRY

No comments:

Post a Comment