KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, January 20, 2016

KALALE PEMA SULEIMAN SAID 'YELSTIN'


KWA kawaida mauti huua mwili wa binadamu ukabaki vumbi tupu kaburini, lakini yale yote mema aliyoyafanya katika kipindi chote alichokuwepo hapa duniani, yatabaki kwenye kumbukumbu milele. Kamwe hayatafutika.

Hivyo ndivyo itakavyokuwa kwa marehemu Suleiman Said Suleiman, maarufu kwa jina la 'Yelstin', ambaye alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).

Yelstin, ambaye aliwahi kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa Simba kati ya mwaka 1997 hadi 1999, alifariki dunia Jumatatu asubuhi, alipokuwa akiogelea katika Bahari ya Hindi na kuzikwa siku hiyo hiyo jioni kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.

Mwanamichezo huyo alipatwa na mauti wakati akipelekwa Hospitali ya Agha Khan, baada ya misuli kukaza ghafla alipokuwa akiogelea katika bahari hiyo, ukiwa ni utaratibu wake wa kawaida wa kila siku asubuhi.

Kwa mujibu wa Mwanasheria Mkuu na Ofisa Uhusiano wa TAA, Ramadhani Maleta, marehemu alikuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi ya kuogelea kila siku wakati wa asubuhi kutoka Feri hadi Kigamboni.

Maleta alisema siku ya tukio, marehemu alikwenda Feri kwa ajili ya kuogelea saa 12 asubuhi, ambapo aliogelea hadi Kigamboni na alipokuwa anarudi, akapatwa na tatizo la kukaza kwa misuli na kuishiwa nguvu.

Ofisa huyo wa TAA amekielezea kifo cha Suleiman kwamba kimeacha pigo kubwa kwa mamlaka hiyo kwa kumpoteza kiongozi mahiri, ambaye hakuwa na majigambo wala kuweka matabaka baina yake na wafanyakazi wenzake.

Marehemu Suleiman atakumbukwa kwa mchango mkubwa alioutoa katika kusimamia ujenzi wa viwanja vya ndege vya Songwe na Mpanda. Pia ndiye aliyekuwa akisimamia ujenzi wa awamu ya tatu wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA).

Kifo cha Suleiman pia kimeacha pigo kubwa katika tasnia ya michezo, hasa mchezo wa soka. Alikuwa shabiki na mwanachama damu wa Simba, ikiwa ni pamoja na kuiongoza miaka ya 1990.

Aliingia Simba akiwa mmoja wa viongozi wa kamati ya muda, iliyokuwa chini ya mwenyekiti, marehemu Saleh Ghulum. Kamati hiyo iliundwa baada ya wanachama kuuondoa madarakani uongozi wa mwenyekiti, marehemu Ismail Kaminambeo na katibu mkuu, marehemu Priva Mtema.

Wakati wote alipokuwa Kaimu Katibu Mkuu wa Simba, marehemu Suleiman alikuwa kiongozi makini na mwenye msimamo. Hakuwa tayari kuyumbishwa na wanachama wakorofi ama wafadhili wa zamani wa klabu hiyo waliokuwa na uwezo mkubwa kifedha.

Hata hivyo, marehemu Suleiman alikuwa tayari kushirikiana na watu wa aina hiyo iwapo misaada yao haikuwa na masharti au dhamira ya kuudhalilisha uongozi wa Simba.

Kuna wakati Simba ilipokuwa ikijiandaa kwenda Kenya kucheza mechi ya kimataifa huku uongozi ukiwa hauna pesa, mmoja wa wakurugenzi wa zamani wa klabu ya Sigara, Kassim Dewji, alijitolea kuigharamia timu hiyo na Suleiman aliukubali msaada huo.

Mbali na Dewji, aliyekuwa Katibu wa Chama cha Soka mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Ismail Aden Rage, naye alijitolea kuisaidia Simba katika safari hiyo na marehemu Suleiman alikuwa tayari kuupokea msaada huo.

Pengine kitu pekee, ambacho Suleiman hakuwa akikifurahia wakati wote alipokuwa kiongozi wa Simba bila kuonyesha waziwazi hisia zake hizo, ni kujazana kwa wanachama maarufu kwa jina la 'makomandoo' ofisini kwake, kuanzia asubuhi hadi jioni.

Tabia hiyo pia haikuwa ikiwafurahisha wafanyakazi wenzake na kila walipowaona wanachama hao, waliwaeleza kwamba Suleiman hakuwepo ofisini na pengine hakutarajiwa kufika kwa siku hiyo.

Lakini cha ajabu ni kwamba kila marehemu Suleiman alipotoka nje ya ofisi yake na kuwakuta wanachama hao nje, aliwaita na kuwasalimia na pengine kuwaachia 'kitu kidogo' kwa wale waliokuwa na matatizo.

Sifa nyingine ya Suleiman ni kutoa ushirikiano kwa vyombo vya habari. Aliwapenda waandishi wa habari na alikuwa tayari wakati wowote kuwapa taarifa walizozihitaji kuhusu Simba.

Hata kama hakuwa na taarifa yoyote ya kuwapa, marehemu Suleiman alipenda kuwakaribisha ofisini kwake au klabuni na kubadilishana nao mawazo kuhusu Simba huku akiwasisitizia kutoandika chochote kuhusu walichozungumza.

Hivyo ndivyo alivyokuwa marehemu Suleiman, aliyeacha mke na watoto watatu. Mungu aipumzishe roho ya marehemu mahali pema.

No comments:

Post a Comment