MCHEZA filamu machachari wa kike nchini, Elizabeth Michael, maarufu kwa jina la Lulu, wiki hii aliwashangaza mashabiki wa fani hiyo baada ya kusema kuwa hana mpenzi na havutiwi na suala la mapenzi kwa sababu umri wake ni mdogo. Lulu alisema hayo alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Mkasi kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha Channel Five. Yafuatayo ni mahojiano ya ana kwa ana kati ya Lulu na mtangazaji wa kipindi hicho, Salama Jabir kama yalivyonukuliwa na mwandishi wetu.
SWALI: Ni kwa nini umekuwa ukiandikwa sana na vyombo vya habari?
JIBU: Hata mimi nashindwa kuelewa! Lakini habari zote zinazoandikwa juu yangu sio za kweli, ni uongo mtupu.
SWALI: Kuna wakati gazeti moja liliwahi kuripoti kwamba ulikuwa na rafiki wa kike msagaji, je habari hizi ni za kweli?
JIBU: Kwa kweli sielewi niseme nini kwa sababu nilipigwa picha nikiwa na dada mmoja klabu, ambaye ninamuheshimu, lakini nikashangaa kuona habari ile.
SWALI: Kuna habari kwamba nyinyi mmekuwa mkiuza stori zenu kwa waandishi wa habari ndio sababu mmekuwa mkiandikwa mara kwa mara, je madai haya yana ukweli wowote?
JIBU: Nasikia vitu hivyo vipo, lakini mimi havijawahi kunitokea. Inavyosemekana wapo wasanii wanaofanya hivyo, lakini sina uhakika.
SWALI: Kwa hiyo unataka kusema kwamba hata wewe umekuwa ukishtukia tu kuona habari zako zinaandikwa magazetini?
JIBU: Ni kweli kabisa na wakati mwingine watu huwa wakinipigia simu kuniuliza, ‘tumeona habari fulani kuhusu wewe’. Huwa zinanishangaza sana.
SWALI: Ni kipi kilichokuvutia na kukufanya upende kuwa mwigizaji filamu?
JIBU: Aliyevumbua kipaji changu ni Dk. Cheni. Ndiye aliyenipeleka katika kikundi cha Kaole wakati huo nikiwa mdogo sana na hatimaye nikajikuta nakuwa mwigizaji.
SWALI : Kwa maana hiyo unataka kusema kwamba uigizaji ni kitu ulichokuwa ukitaka kukifanya kwa muda mrefu?
JIBU: Kwa kweli sikuwa na ndoto hiyo. Sikufikiria iwapo siku moja nitakuwa staa. Sikuona kama ni kazi. Nilikuwa nikisikia raha tu kuigiza.
SWALI : Kuna gazeti moja liliwahi kuripoti hivi karibuni kwamba una uhusiano wa kimapenzi na Ali Kiba. Je, kuna ukweli wowote kuhusu habari hii ?
JIBU: Hapana, ndio maana uliposoma hilo gazeti, hukuona picha imechapishwa ikimuonyesha Lulu na Kiba. Kama habari hiyo ingekuwa ya kweli, lazima kungekuwepo na picha inayomuonyesha Lulu na Kiba. Kwangu mimi Ali Kiba ni rafiki yangu wa kawaida tu.
SWALI: Inasemekana kwamba watayarishaji wengi wa filamu wamekuwa wakitengeneza sehemu ya kwanza na ya pili kwa lengo la kupata pesa, yaani wanawaibia mashabiki. Je, kuna ukweli wowote kuhusu madai hayo ?
JIBU: Mimi nadhani inategemea na stori ya mtu. Zingine zinastahili kuwa na sehemu ya kwanza na ya pili na zingine hazistahili. Kibaya zaidi nyingi hazina kiwango. Kwa sasa hatuna uwezo huo, tunajaribu tu.
Kwa mfano, mimi kwa wakati huu natengeneza filamu yangu, lakini sina uwezo wa kuifanya iwe ya kiwango cha juu. Lakini nitajaribu kuifanya iwe na mvuto ili lengo langu litimie.
SWALI : Kuna madai kwamba baadhi yenu waigizaji nyota hampendi kuigiza nafasi za watumishi wa ndani ama zingine za kiwango cha chini. Kuna ukweli wowote kuhusu hili ?
JIBU: Sipendi kuwasemea wengine, lakini kwa upande wangu, naweza kuigiza nafasi yoyote kwa sababu nina uwezo wa kufanya hivyo.
SWALI : Hebu tuambie, unao wapenzi wangapi wa kiume?
JIBU: Jamani, sina mpenzi, mimi ni mwanamke singo na umri wangu bado mdogo kuwa na mwanaume. Nina miaka 18 tu.
SWALI : Tafadhali zungumza ukweli maana kwa msichana kama wewe unaweza kuwa na wanaume wa aina tofauti, huyu wa kununua vocha, huyu wa kununua mavazi, huyu wa kununua gari na huyu mtoa huduma. Unataka kutuambia hilo gari lako aina ya Lexus limekuja lenyewe ?
JIBU: Hivi kwa sababu gani humtaki kuniamini? Tatizo nini? Vitu vyote hivi navipata kutoka kwa mama yangu.
SWALI : Unataka kutuambia kwamba mama yako ndiye anayekupa pesa za kwenda saluni, kununua nguo za bei mbaya na kununua gari?
JIBU: Kuna habari pia kuwa baadhi yenu huwa mnapenda sana wanaume watu wazima je, ni kweli ?
JIBU: Ni kweli wapo wanawake wa aina hiyo, lakini kwangu mimi hapana.
SWALI: Hebu tueleze kuhusu maisha yako, wewe ni mtu wa aina gani ?
JIBU : Mimi ni mtu wa kawaida tu, naishi maisha ya kawaida na ninaongea na kila mtu.
SWALI : Ni kweli kwamba baadhi yenu wacheza filamu wa kike huwa hampewi nafasi ya kucheza filamu hadi utembee na watayarishaji wa filamu wanaume kama vile Ray na Kanumba ? JIBU: Siwezi kulizungumia hilo kwa sababu halijawahi kunitokea.
SWALI : Ni kwa nini ulifikiria kuanza kutengeneza filamu zako mwenyewe ? Inawezekana ni kwa sababu uliona malipo unayoyapata kwa kucheza filamu hayatoshi ?
JIBU: Niliona nimeshacheza filamu nyingi na nimeshapata uzoefu na pia nina kipaji.
SWALI : Nini matarajio yako ya baadaye ?
JIBU : Kwa sasa nataka niendelee na shule. Unajua mimi nilimaliza kidato cha nne na shule ndiyo kila kitu. Nimejiwekea malengo ya kufika mahali fulani katika maisha yangu.
SWALI : Unaweza kupika chakula wewe ?
JIBU : Kwa nini nisiweze ? Naweza kupika vyakula vya aina zote, napiga ugali, wali, pilau na vinginevyo.
SWALI : Katika familia yenu mpo wangapi ?
JIBU: Tupo wawili, mimi na mdogo wangu. Tumelelewa zaidi na mama.
SWALI: Ni filamu gani iliyowahi kukusumbua sana tangu ulipoanza kucheza filamu?
JIBU: Kuna movi moja hiyo siwezi kuisahau, tulikuwa tunakimbia porini pekupeku na kuchomwa na miiba. Tuliigiza sehemu moja hivi kule Kibaha.
SWALI: Ni kiasi gani cha pesa, ambacho umekuwa ukilipwa kwa kucheza filamu moja?
JIBU: Unataka nikueleze siri yangu? Ni malipo ya kawaida tu ya kumwezesha mtu aweze kumudu maisha yake ya kila siku.
SWALI: Umeshamaliza kutengeneza filamu yako? Umetumia gharama kiasi gani kuanzia mwanzo hadi mwisho na je, imeshaingia sokoni?
JIBU: Filamu yangu imeshamalizika, lakini bado haijaingia sokoni. Nimetumia fedha nyingi tu kuitengeneza.
SWALI: Unaionaje kazi ya kucheza filamu?
JIBU: Naifurahia sana, najisikia raha kucheza filamu.
SWALI: Mbali na kucheza filamu, kitu gani kingine unachokipenda katika maisha yako?
JIBU: Napenda kuimba na kucheza.
SWALI : Ungependa kuwa mwanamuziki siku moja ?
JIBU : Ndio
SWALI : Unadhani muziki unakupenda au wewe ndio unaupenda ?
JIBU : Utanipenda tu.
No comments:
Post a Comment