KOCHA Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic amegoma kusafiri na timu hiyo kwenda Mwanza baada ya kuweka mgomo bardi, kufuatia viongozi wa timu hiyo kukwepa kukutana naye.
Habari zilizopatikana jana kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, kocha huyo amechukizwa na hatua ya viongoziwa klabu yake kugoma kukutana naye ili kuzungumzia hatma yake.
Yanga iliondoka mjini Dar es Salaam jana kwenda Mwanza, ambako Jumapili ijayo itacheza na Toto African katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, itakayopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
Kocha huyo kutoka Serbia anatarajiwa kumaliza mkataba wake Aprili 23 mwaka huu na taarifa zisizo rasmi zimeeleza kuwa, tayari uongozi wa Yanga umeshaanza kusaka kocha mwingine.
Hata hivyo, akizungumzia suala la kocha huyo, Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Papic hakwenda Mwanza kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya tumbo, homa na mapafu.
Sendeu alisema Papic alianza kuugua siku tatu zilizopita na madaktari wamemshauri asisafiri safari ya masafa marefu kwa vile bado hajapona sawasawa.
Kwa mujibu wa Sendeu, kikosi cha Yanga kimekwenda huko kikiwa chini ya Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Fred Felix Minziro.
Sendeu alisema Yanga inatarajiwa kucheza mechi moja ya kirafiki itakayochezwa Kahama mkoani Shinyanga dhidi ya timu ya Ambassador kabla ya kuondoka kesho kwenda Mwanza. Katika msafara huo, mshambuliaji Hamizi Kiiza aliachwa kutokana na kuchelewa kuungana na wenzake, lakini anatarajiwa kuondoka leo na kwenda moja kwa moja Mwanza.
No comments:
Post a Comment