KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, April 28, 2012

JAMAL BAYSER: Ipo siku mechi za ligi kuu zataleta maafa


WAKATI michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara msimu huu ikiwa inaelekea ukingoni, mratibu wa timu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro, Jamal Bayser ameonya kuwa, iwapo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) haitakuwa makini, ipo siku mechi za ligi hiyo zitasababisha maafa. Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na Mwandishi Wetu, ATHANAS KAZIGE, kiongozi huyo wa Mtibwa Sugar anafafanua kuhusu tahadhari yake hiyo.

SWALI: Michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara msimu huu inaelekea ukingoni. Una jambo gani ambalo ungependa kulizungumza kuhusu ligi hiyo?
JIBU: Katika msimu huu wa ligi nimeweza kujionea mambo mengi ya ajabu, ambayo kama hatua za haraka hazitachukuliwa, ipo siku huenda tukapata hasara kubwa.
Nasema hivyo kutokana na kuwepo kwa mambo ya kusikitisha, ikiwa ni pamoja na baadhi ya timu kubwa kubebwa na waamuzi na kusababisha hali ya utulivu katika mchezo wa soka kutoweka.
Nina hakika iwapo hatua hizo zitachelewa kuchukuliwa, ipo siku tutashuhudia waamuzi wetu wakisababisha umwagikaji wa damu katika viwanja vya soka na hivyo kulitia doa jina la Tanzania katika ramani ya soka ulimwenguni.
SWALI: Kwanini unasema hivyo?
JIBU: Unajua hakuna kitu kibaya kama ushabiki ndani ya soka. Kila timu inaingia gharama kubwa kusajili wachezaji, kulipa mishahara,
kuwalipia matibabu wachezaji na mambo mengine mengi, ambayo huchangia kuzifanya timu zetu ziendelee kuwepo. Lakini unapofika uwanjani, unakutana na madudu ya ajabu. Inauma sana.
Unavyoiona timu kama Mtibwa Sugar, unajua inatumia pesa nyingi, lakini inapata mapato kidogo kutokana na mechi za ligi na za wadhamini, lakini lengo kubwa tunataka tufanye vizuri kwa kupata ushindi.
Sasa unapofika uwanjani na kuona timu yako inaonewa na ile isiyokuwa na uwezo inashinda, kwa kweli inauma sana. Fikiria ungekuwa ni wewe ungejisikiaje? Mnatumia pesa nyingi kuihudumia timu, halafu mnafungwa kwa sababu ya hila za wapinzani wenu.
Ndio sababu nimesema kuwa, inabidi TFF wafanye maamuzi magumu kuhusu waamuzi na timu ambazo zimekuwa zikibebwa kutokana na kutumia mbinu chafu kwa sababu mtindo huu umekuwa ukizidi kuota mizizi na hakuna hatua zozote zinazochukuliwa kwa wahusika.
Timu kama Azam imekuwa ikilalamikiwa na timu nyingi. Tayari
Yanga,Villa Squad, Polisi Dodoma zimeshatoa malalamiko kuhusu Azam na sasa sisi Mtibwa Sugar kutokana na mechi zao kutawaliwa na mbinu chafu na kujitokeza kwa vitendo vya vurugu.
Kwa kweli mashabiki wa timu nyingi za ligi kuu wamekuwa wavumilivu, lakini ipo siku uvumilivu wao unaweza kufikia kikomo na kuamua kuingia uwanjani kufanya vurugu na hatimaye damu kumwagika. Lazima TFF ichukue tahadhari mapema.
SWALI: Unadhani nini kifanyike ili kuondoa tatizo hilo, ambalo umelielezea kuwa kwa sasa limekuwa sugu?
JIBU: Mimi binafsi nafikiri kwamba umefika wakati kwa TFF kuhakikisha kila mchezo unarekodiwa ili matukio yote ya uwanjani yaweze kuonekana na kama kuna pingamizi lolote haki iweze kutendeka.
Nasema hivyo kwa sababu hali imekuwa mbaya sana. Kila kukicha watu au viongozi wa baadhi ya timu wamekuwa wakiwalalamikia waamuzi wetu kwa kushindwa kuzitumia vyema sheria 17 za soka.
Pia napenda zitungwe sheria kali kwa yoyote, ambaye atashindwa au kuthibitika amepewa rushwa na timu au kiongozi ili liweze kuwa fundisho kwa watu wengine wenye tabia hiyo.
Nina hakika iwapo itatokea mwamuzi mwingine anafungiwa maisha au kupigwa faini au kufungwa jela kutokana na kupokea rushwa,
litakuwa funzo kubwa kwa wengine na hata kupunguza vitendo hivyo katika soka.
SWALI: Una maoni gani kuhusu utendaji wa TFF? Au tuseme kuna kasoro nyingine yoyote uliyoibaini zaidi ya waamuzi?
JIBU: Mimi naona zipo changamoto chache ndani ya TFF. Miongoni mwa changamoto hizo ni kuwepo kwa mikakati ya kusaka wadhamini zaidi kwenye ligi hiyo na ile ya taifa.
Sio siri, unajua hali ya kifedha ni ngumu kwa baadhi ya timu. Klabu nyingi zina hali mbaya na hata pesa za mdhamini wa ligi hiyo, Vodacom hazitoshi. Inabidi TFF ifanye kazi ya kusaka wadhamini wengine.
Sambamba na jambo hilo, napenda TFF wawekeze nguvu zaidi katika timu za vijana na ikiwezekana waanzishe ligi yao na kuwatafutia wadhamini ili kuongeza ushindani na hapo watakuwa wanakuza mchezo huo.
SWALI: Kikosi cha Mtibwa Sugar msimu huu kimekuwa hakifanyi vizuri katika michezo mbalimbali. Unaweza kueleza tatizo hasa ni nini?
JIBU: Sio kweli kwamba kikosi chetu hakifanyi vizuri. Tumekuwa tukifanya vizuri katika mechi nyingi, isipokuwa yapo baadhi ya matatizo kama vile baadhi ya wachezaji kuwa majeruhi kwa kipindi kirefu na wengine viwango vyao kushuka. Lakini sababu kubwa ni waamuzi kutotutendea haki katika mechi zetu.
Nasema hivyo kwa sababu msimu huu umetawaliwa na mambo mengi ya ajabu. Kila kukicha, timu nyingi zinasaka pointi tatu kwa hila mbalimbali na gharama kubwa. Kwetu sisi hilo jambo halipo kabisa.
Lakini bado tunayo nafasi ya kufanya mabadiliko kwenye kikosi chetu na kitaweza kufanya vizuri msimu ujao, ingawa najua wazi kwamba kazi hiyo itakuwa ngumu.
Benchi letu la ufundi linafanya kazi yake vizuri kuhusu suala hilo kwa kipindi hiki kwa kuangalia mchango wa kila mchezaji na litaleta kwetu
mapendekezo yake ili tuweze kuyafanyia kazi na kujenga kikosi imara na cha ushindi msimu ujao.
SWALI: Katika miaka ya nyuma ulikuwa mmoja wa viongozi wa juu wa TFF. Je, una mpango wowote wa kugombea uongozi katika uchaguzi ujao wa shirikisho hilo unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu?
JIBU: Swali lako ni sana. Ukweli ni kwamba kwa sasa nina kazi nyingi sana, lakini pia ni mapema mno kuzungumzia jambo hilo, ingawa sina mawazo ya kufanya hivyo.

No comments:

Post a Comment