MSANII nyota wa filamu nchini, Jacob Steven, maarufu kwa jina la JB, amesema hatatokea kiongozi wa nchi mwenye mapenzi na wasanii kama ilivyo kwa Rais Jakaya Kikwete.
JB amesema mbali ya kuwapenda wasanii wa fani zote, Rais Kikwete amekuwa mstari wa mbele kupenda kazi zao na kutaka wanufaike na vipaji vyao.
Msanii huyo alisema hayo siku moja kabla ya mazishi ya nguli wa fani ya filamu nchini, marehemu Steven Kanumba yaliyofanyika juzi kwenye makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.
“Natamani Rais Kikwete angekuwa kiongozi wa milele wa Tanzania! Jamani, sijawahi kuona kiongozi anayewajali wasanii kama Kikwete,”alisema.
JB alimwelezea Rais Kikwete kuwa ni mtu anayependa kufuatilia kazi za wasanii wa nchi yake na katika kudhihirisha mapenzi yake kwao, amekuwa akiwaalika mara kwa mara Ikulu na kula nao chakula.
“Unaweza kupenda kuangalia kazi za wasanii, lakini usiwajali, lakini kwa Rais Kikwete, anapenda vyote, hatuna budi kumshukuru na kuongeza bidii katika kazi zetu,”alisema.
Msanii huyo pia alielezea kuguswa na uamuzi wa Rais Kikwete kushirikiana bega kwa bega na familia ya marehemu Kanumba pamoja na wasanii wa filamu wakati wote wa msiba wa mwigizaji huyo.
Alisema akiwa kiongozi mkuu wa nchi, Rais Kikwete aliacha shughuli zake zote na kwenda nyumbani kwa marehemu Kanumba kuwapa pole wafiwa na pia kuzungumza machache na wasanii.
“Ni viongozi wachache wenye moyo na sifa za aina hiyo. Tunapaswa kumshukuru na kumpongeza rais wetu kwa ukaribu aliouonyesha kwetu wasanii,”alisema.
Kanumba alifariki dunia Aprili 6 mwaka huu nyumbani kwake Sinza, Dar es Salaam baada ya kutokea ugomvi kati yake na msanii mwenzake wa filamu, Elizabeth Michael ‘Lulu’.
Mazishi ya Kanumba, ambayo yameelezewa kuwa ni ya kihistoria yalifanyika juzi kwenye makaburi ya Kinondoni na kuhudhuriwa na maelfu ya watu, wakiongozwa na Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal.
Akiwa nyumbani kwa marehemu Kanumba alikokwenda kuwapa pole wafiwa, Rais Kikwete aliahidi kuwa, ataendelea kuwa bega kwa bega na wasanii ili kuhakikisha wanafaidi matunda ya jasho lao.
Rais Kikwete alisema ametoa maelekezo kwa JB na baadhi ya wasanii wenzake alipowaita Ikulu mjini Dar es Salaam hivi karibuni na kwamba anasubiri mrejesho kutoka kwao ili akamilishe azma yake ya kuwasaidia kimaendeleo.
Katika kikao chake na wasanii hao, Rais Kikwete aliwataka waeleze changamoto mbalimbali zinazowakabili ili aweze kuwasaidia na kutatua matatizo yao.
JB alisema kauli hiyo ya Rais Kikwete inaonyesha dhahiri kwamba, amepania kwa dhati kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili wasanii wa fani hiyo, ikiwa ni pamoja na kuibiwa kazi zao na wafanyabiashara.
Hata hivyo, JB alisema mazungumzo hayo yaliyodumu kwa saa tatu yatazaa matunda iwapo tu yeye na wasanii wenzake watakuwa kitu kimoja na kuondoa tofauti zilizopo kati yao.
Kauli hiyo ya JB imekuja siku chache baada ya msanii mwingine wa fani hiyo, hasa vichekesho, Steve Mengere ‘Nyerere’ kutamka kuwa, wasanii watamkumbuka Rais Kikwete baada ya kuondoka madarakani.
Msanii huyo mahiri kwa kuigiza sauti ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere alisema, binafsi amepata mafanikio makubwa kiusanii baada ya kuingia madarakani Rais Kikwete.
“Mimi nasema Rais Kikwete akiondoka madarakani, wasanii watamkumbuka sana kwa sababu haijawahi kutokea na haitatokea kiongozi wa nchi anayependa sanaa kama JK,”alisema.
Aliitaja faida nyingine aliyoipata kiusanii tangu JK alipoingia madarakani kuwa ni kupata nafasi ya kukaa naye karibu na pia kula naye chakula.
“Lakini kikubwa zaidi ni Rais Kikwete kujua kwamba kuna mtu anaitwa Steve Nyerere,”alisema msanii huyo mwenye vituko na makeke.
Hata hivyo, Steve alikiri kuwa ni vigumu kwa wasanii nchini kupata mafanikio makubwa kiusanii kutokana na kutokuwa na umoja. Alisema sababu kubwa inayowafanya wasanii wasiwe na msimamo ni njaa.
“Wasanii hatuna viwango maalumu vya malipo kwa kazi tunazozifanya. Wewe ukikataa malipo ya shilingi 500,000 kwa kuona ni kiwango kidogo, mwenzako atapokea. Na ukitaka ulipwe shilingi milioni moja, utakufa na njaa,”alisema.
No comments:
Post a Comment