KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 5, 2012

KABURU: Lazima tuishinde ES Setif

KIKOSI cha timu ya soka ya Simba kiliondoka nchini Jumatatu iliyopita kwenda Algeria kwa ajili ya mechi ya marudiano ya michuano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya ES Setif ya huko inayotarajiwa kuchezwa kesho mjini Setif. Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na Mwandishi Wetu, ATHANAS KAZIGE, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ anaelezea mikakati na matumaini yao katika mechi hiyo.
SWALI: Kikosi chenu kimeshaondoka nchini kwenda Algeria kwa ajili ya mechi yenu ya marudiano dhidi ya ES Setif, itakayochezwa Ijumaa. Mmejipanga vipi kuhakikisha kuwa mnashinda mechi hiyo?
JIBU: Tumejipanga vizuri. Kwanza kabisa viongozi tumefanya kazi yetu ya utawala kwa umakini mkubwa na kila kitu kuhusu Simba kwenda Algeria kimekwenda vizuri.
Unajua safari ni hatua, hivyo tumejipanga kwenda katika vita ya marudiano, ambayo tuna hakika itakuwa ngumu kwetu kwa vile wapinzani wetu hawatakuwa tayari kufungwa nyumbani kwao tena mbele ya mashabiki wao.
Pamoja na ukweli huo, sisi kama viongozi tulishawasiliana na ubalozi wa Tanzania uliopo Algeria kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri na tayari baadhi ya viongozi wetu wa kamati ya ufundi walishatangulia huko.
SWALI: Nimemsikia mwenyekiti wenu Ismail Aden Rage akisema kwamba, wapo baadhi ya Watanzania wanaoishi nchini Algeria, ambao wameahidi kuwashangilia kwa nguvu zote wakati wa mechi hiyo. Je, taarifa hizo ni za kweli?
JIBU: Habari hizo ni za kweli. Wapo watanzania wengi kule Algeria, ambao wameahidi kutuunga mkono. Kwa maana hiyo, Simba itakwenda Algeria ikiwa haina wasiwasi wa kukosa kuungwa mkono.
Kule Algeria wapo wanafunzi wengi kutoka hapa nchini, ambao wamekwenda huko kusoma katika vyuo mbalimbali. Watanzania hao ndio waliotuahidi kutuunga mkono katika mechi hiyo.
SWALI: Mmepanga kusimama kwa muda Misri kwa ajili ya kujipanga kabla ya kwenda Algeria. Lengo lenu ni lipi hasa ?
JBU: Tumeamua kusimama Misri kwa muda kwa ajili ya kufanya mazoezi angalau kwa siku moja na kisha siku inayofuata, tutaondoka kwenda Algeria. Sababu hasa ya kusimama kwa muda Misri ni kutaka kuzoea hali ya hewa ya huko, ambayo inafanana na ile ya Algeria.
Nina hakika wachezaji wetu wataweza kuizoea hali hiyo ya hewa haraka ili waweze kukabiliana vyema na wapinzani wenu. Tumefanya hivyo kwa sababu tulipata tabu sana tulipokwenda Rwanda kucheza na Kiyovu katika mechi ya raundi ya kwanza.
SWALI: Kuna wakati Rage alitoa ahadi ya kuwashonea suti wachezaji wote wa Simba. Je, ameshatimiza ahadi hiyo kabla ya timu kuondoka kwenda Algeria?
JIBU: Ni kweli, tayari wachezaji wetu wote pamoja na viongozi wa benchi la ufundi wameshapata suti hizo na walizivaa siku walipoondoka kwenda Algeria.
Lengo la uongozi kuwanunulia suti wachezaji ni kuipa timu heshima yetu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Klabu zetu zinapaswa kubadilika hivi sasa kwa kwenda na wakati. Tunapaswa kuwavalisha wachezaji wetu nguo za heshima ili waonekane kuwa na thamani mbele ya watu.
Tumepanga kuendelea kufanya mambo makubwa zaidi katika mechi zetu zijazo na hilo litaonekana hapo baadaye. Tunataka wachezaji wetu waweze kujitambua kwamba wapo kwenye klabu kubwa, ambayo inahitaji kuheshimiwa, si kimchezo tu, bali hata kwa mavazi.
SWALI: Kuna ahadi yoyote mliyotoa kwa wachezaji wenu ili kuwahamasisha waweze kushinda mechi hiyo?
JIBU: Ahadi ya zawadi ipo, lakini hiyo ni siri ya klabu, hatuwezi kuitangaza kwa vile ni mambo ya ndani ya klabu yetu ya Simba.
SWALI: Nini maoni yako kuhusu mwenendo wa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara, ambayo kwa sasa inaelekea ukingoni?
JIBU: Ligi ya msimu huu ni ngumu ndio sababu hadi sasa hakuna timu yenye uhakika wa kuibuka na ubingwa. Ushindani bado ni mkubwa kwa timu tatu za kwanza na yoyote itakayoshinda mechi zilizosalia, inaweza kutwaa ubingwa.
Pengine jambo la msingi ningependa kuwaomba waamuzi wa ligi hiyo waheshimu na kuzingatia sheria 17 za soka ili washindi waweze kupatikana kutokana na uwezo wao uwanjani badala ya kubebwa.
SWALI: Unauelezeaje ushindani uliopo kati yenu, Yanga na Azam katika kuwania ubingwa?
JIBU: Kwa maoni yangu, naweza kusema kwamba mchuano ni mkali na tunaendelea kupambana ili kuhakikisha tunaivua ubingwa Yanga. Hilo linawezekana kwa vile ndani ya kikosi chetu kuna ushirikiano mkubwa kati ya wachezaji, viongozi na benchi la ufundi.

No comments:

Post a Comment