KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, April 18, 2012

MBUNGE AMUUMBUA WAZIRI BUNGENI

MBUNGE wa Kinondoni, Iddi Azzan amemuumbua Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukandala kwa kutoa taarifa potofu.
Azzan amesema pia kuwa, amesikitishwa na majibu yaliyotolewa na serikali, ambayo hayakuwa sahihi na kuongeza kuwa, huenda haikufanya utafiti kutokana na kile ilichoulizwa.
Mbunge huyo alitoa malalamiko hayo bungeni jana baada ya majibu ya Dk. Fennela kwa Ahmed Juma Ngwali (Ziwani), aliyetaka kufahamu mafanikio ya msingi liliyopata Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) tangu lilipojiunga na Shirikisho la Soka Dunia (FIFA) mwaka 1964.
Akijibu swali hilo, Dk. Fenella alisema TFF imepata mafanikio mengi ya msingi, ikiwemo kukuza na kuendeleza mpira wa miguu nchini pamoja na kuweka muundo wa utawala katika ngazi zote ambao unatekelezeka.
Naibu waziri alisema pia kuwa, TFF imeandaa na kuendesha programu mbalimbali ikiwa ni pamoja na mashindano ya timu za vijana, wanawake na watoto kama sehemu ya kuweka misingi bora ya maendeleo ya soka.
Alisema katika kipindi hicho, timu ya taifa iliweza kutwaa kombe la Chalenji mara tano huku klabu za Simba na Yanga zikinyakua Kombe la klabu bingwa Afrika Mashariki mara moja kila mmoja.
Mara baada ya majibu hayo, Azzan alisimama na kuomba kutoa taarifa, ambapo Naibu Spika wa Bunge alimtaka kuvuta subira kwanza.
Alipopewa nafasi hiyo, Azzan alisema majibu yaliyotolewa na serikali kupitia Dk. Fennela si sahihi kwa vile si kweli kwamba Simba na Yanga zimenyakua ubingwa wa Afrika Mashariki mara moja kila moja.
Alisema Simba imenyakua ubingwa huo mara sita, Yanga mara tano na timu ya Taifa imebeba Kombe la Chalenji mara tatu.
“Majibu ya serikali yanasikitisha mno na nadhani hayajafanyiwa utafiti,” alisema mbunge huyo na kuufanya ukumbi kuwa kimya.

No comments:

Post a Comment