SIMBA jana ilizidi kujisafishia njia ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa JKT Ruvu mabao 3-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wakati Simba ikiibuka na ushindi huo mnono, watani wao wa jadi Yanga jana walichapwa bao 1-0 na Kagera Sugar katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Kwa matokeo hayo, Simba inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 56 baada ya kucheza mechi 24, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 50. Yanga ni ya tatu ikiwa na pointi 43.
Simba sasa inahitaji kuishinda Moro United zitakapomenyana Aprili 25 mwaka huu ili ijihakikishie kutwaa taji hilo, lakini itategemea zaidi matokeo kati ya Azam na Mtibwa zitakazomenyana Jumamosi.
Iliwachukua Simba dakika moja kuhesabu bao la kwanza lililofungwa na Uhuru Selemani baada ya kupokea pasi maridhawa kutoka kwa Emmanuel Okwi.
Haruna Moshi ‘Boban’ aliifungia Simba bao la pili dakika ya 17 baada ya kuwapiga chenga viungo na mabeki wa JKT Ruvu kabla ya kufumua shuti kali lililopita kushoto kwa kipa Amani Simba.
Simba ilipata nafasi zingine nzuri za kufunga mabao dakika ya 35 na 41 baada ya Uhuru na Kago kupewa pasi wakiwa ndani ya eneo la hatari, lakini mipira waliyopiga ilitoka nje ya lango la JKT.
JKT Ruvu ilipata nafasi pekee nzuri ya kufunga bao dakika ya 44 wakati Hussein Bunu alipopewa pasi murua na Mohamed Banka huku kipa Juma Kaseja wa Simba na mabeki wake wakiwa wamepoteana, lakini shuti lake lilitoka nje.
Bao la tatu la Simba lilifungwa na Mwinyi Kazimoto dakika ya 64 baada ya kuunganisha wavuni kwa shuti kali la mbali mpira wa adhabu ndogo.
Habari kutoka Bukoba zimeeleza kuwa, bao pekee na la ushindi la Kagera Sugar lilifungwa na Shija Mkina katika kipindi cha pili.
Kipigo hicho kilikuwa cha pili kwa Yanga katika muda wa siku nne baada ya mwishoni mwa wiki iliyopita kupigwa mweleka wa mabao 3-2 na Toto African mjini Mwanza.
SIMBA: Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Amir Maftah, Juma Nyoso, Kevin Yondan, Patrick Mafisango, Uhuru Selemani, Mwinyi Kazimoto, Gervas Kago, Haruna Moshi ‘Boban’ na Emmanuel Okwi.
JKT Ruvu: Amani Simba, Kessy Mapande, John Mhidze, Hassan Kikutwa, George Minja, Jimmy Shoti, Haruna John, Nashon Matari, Hussein Bunu, Mohamed Banka/George Mketo na Emmanuel Pius.
No comments:
Post a Comment