HALI imeanza kuwa si shwari ndani ya klabu ya Yanga baada ya baadhi ya wanachama na wazee wa klabu hiyo kushinikiza Katibu Mkuu, Selestine Mwesigwa na Mkurugenzi wa Ufundi, Mohamed Bhinda wajiuzulu.
Wakizungumza makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani mjini Dar es Salaam jana, wanachama na wazee hao walidai kuwa, viongozi hao wawili wa Yanga wanapaswa kuwajibika.
Shinikizo la wazee na wanachama hao limekuja siku moja baada ya Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kubariki Yanga kupokwa pointi tatu na Kamati ya Ligi.
Kamati ya Ligi ilifikia uamuzi huo baada ya Yanga kumchezesha beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ katika mechi yao ya ligi kuu dhidi ya Coastal Union iliyochezwa Machi 31 mwaka huu mjini Tanga wakati alikuwa na kadi nyekundu na alipaswa kukosa mechi tatu.
Wanachama hao, ambao hawakutaka majina yao yatajwe gazetini walidai kuwa, uamuzi wa kamati ya nidhamu na usuluhishikuipoka Yanga pointi tatu ni uthibitisho wa wazi wa viongozi hao kushindwa kutekeleza vyema majukumu yao.
Walisema akiwa mkurugenzi wa ufundi, Bhinda hakupaswa kumruhusu beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ acheze mechi hiyo kutokana na kuwa na kadi hiyo nyekundu wakati yeye ndiye anayetunza rekodi zote za wachezaji.
“Huu ni uzembe wa hali ya juu na hatuwezi kuuvumilia, hivyo ni vyema Bhinda awajibike mara moja badala ya kusubiri kutimuliwa,”alisema.
Mmoja wa wanachama hao alisema, Mwesigwa naye anapaswa kuondoka madarakani kwa madai kuwa, amekaimu nafasi hiyo kwa miezi sita bila kuthibitishwa na wanachama na hivyo kukiuka katiba ya klabu hiyo.
Wanachama hao pia walihoji uamuzi wa Bhinda kukodi basi kwa ajili ya kuisafirisha timu kwenda Mwanza wakati wangeweza kutumia basi la klabu hiyo lililotolewa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
Wamemtaka Mwenyekiti wa klabu hiyo, Lloyd Nchunga kuitisha haraka mkutano wa wanachama ili waweze kujadili masuala mbalimbali, ikiwemo kupokwa pointi kwa timu hiyo katika mechi yake dhidi ya Coastal Union.
Nchunga hakuweza kupatikana jana kuzungumzia madai hayo ya wanachama kutokana na simu yake kutopokelewa wakati simu ya Mwesigwa ilikuwa haipatikani.
No comments:
Post a Comment