KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 12, 2012

MAMA LULU: Acheni kumuhukumu mwanangu

Mama mzazi wa msanii Elizabeth Michael 'Lulu', anayedaiwa
kusababisha kifo cha msanii Steven Kanumba, Lucresia Kalugila
amewaomba wanaharakati wamsaidie binti yake ili haki itendeke.
Mama huyo alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza katika
kipindi cha Wanawake Live kilichorushwa hewani na kituo cha
televisheni cha East Africa.
Ameitaka jamii iache kumtupia lawama Lulu kutokana na kifo hicho
cha Kanumba, badala yake wasubiri vyombo vya dola vifanye kazi
yake.
"Kutokana na uzito wa tukio hili, nawaomba wanaharakati
wanawake waniunge mkono ili wanisaidie katika suala hili kwa
kuhakikisha haki inatendeka kwa mtoto wangu,"alisema.
Lucresia alisema binafsi amesikitishwa na kifo cha Kanumba kwa
vile hakutegemea iwapo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na
binti yake. Alisema wote wawili alikuwa akiwaona kama watoto
wake wa kuwazaa.
"Siku zote Kanumba alikuwa akiniita mama, sikuwa na imani
kwamba angeweza kuwa na uhusiano na Lulu, lakini kwa vile
limeshatokea, tuache sheria ichukue mkondo wake,"alisema.
Aliongeza kuwa, si busara kwa baadhi ya watu kwenda kwa mama
mzazi wa marehemu Kanumba kuzungumza maneno ya uongo
dhidi ya binti yake bila kuwa na uhakika wa kile anachokisema.
"Siku ya tukio walikuwepo Kanumba na Lulu, iweje watu wengine
waanze kuzusha maneno wasiyokuwa na uhakika nayo. Tuache
vyombo vya dola vifanyekazi na kutupa majibu,"alisema.
Mama huyo pia alivitaka vyombo vya habari kuripoti habari za
uhakika kwani si kweli kwamba mtoto wake alitaka kwenda
makaburini kwa ajili ya kuuaga mwili wa Kanumba.
"Lulu yupo kituoni chini ya ulinzi wa polisi, iweje leo atake kwenda
msibani kumuaga Kanumba?" Alihoji mama huyo.
Lucresia alisema yupo pamoja na Mama Kanumba kwa vile msiba
huo ni wa wote hivyo amemtaka awe na moyo wa subira na
ustahamilivu kwa vile ukweli utajulikana.
"Mzazi mwenzangu kuwa na subira, tupo pamoja, Kanumba ni
mtoto wetu sote na mimi nina machungu na kifo chake,"alisema.

No comments:

Post a Comment