'
Saturday, April 28, 2012
Niyonzima aiweka Yanga njia panda
MJUMBE wa kamati ya utendaji ya klabu ya Yanga, aliyetangaza kujiuzulu, Abdallah Bin Kleb ametoboa siri kuwa, klabu hiyo inakabiliwa na hali mbaya kifedha.
Wakati Bin Kleb akidai klabu hiyo ina hali mbaya kipesa, kiungo Haruna Niyonzima ameiweka njia panda baada ya kukerwa na uamuzi wa uongozi kumkata pesa zake zote za mshahara.
Bin Kleb amesema hali mbaya ya kifedha inayoikabili Yanga ni sawa na kusema kwamba, imefilisika.
Tajiri huyo aliyemsajili kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Niyonzima alisema hayo mjini Dar es Salaam juzi alipotakiwa kufafanua kuhusu sababu za uamuzi wake wa kujiuzulu.
Bin Kleb alisema Yanga imefilisika kutokana na kuwepo kwa usiri mkubwa kuhusu taarifa za mapato na matumizi ya klabu hiyo.
Alisema wafadhili wengi wamekuwa wakitoa pesa zao mifukoni kwa ajili ya kuisaidia Yanga, lakini hawapewi taarifa kuhusu matumizi yake kutoka kwa uongozi.
Bin Kleb amekuwa mjumbe wa tatu wa kamati ya utendaji ya Yanga kutangaza kujiuzulu. Wengine ni Sara Ramadhani na Seif Ahmed, maarufu kwa jina la Magari.
Kuna habari kuwa, wajumbe wengine wawili wa kamati hiyo huenda wakatangaza kujiuzulu leo. Wajumbe hao ni Ally Mayay na Mzee Yusuph.
Wajumbe wengine wanaounda kamati ya utendaji ya Yanga ni Tito Osoro, Mohamed Bhinda, Charles Mngodo, Salum Rupia na marehemu Theonest Rutashoborwa.
Kwa mujibu wa katiba ya Yanga, iwapo wajumbe watano wa kamati ya utendaji watajiuzulu, itabidi uitishwe mkutano mkuu wa dharula kwa ajili ya kujadili hali hiyo na kuchukua hatua.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, David Mosha alishatangaza kujiuzulu wadhifa huo tangu mwaka jana baada ya kutofautiana na mwenyekiti wake, Lloyd Nchunga.
Nchunga amekuwa akikabiliwa na shinikizo kubwa la kumtaka ajiuzulu, kufuatia mwenendo usioridhisha wa Yanga katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara, inayotarajiwa kufikia tamati Mei 5 mwaka huu.
Wakati huo huo, kiungo Haruna Niyonzima wa Yanga huenda akafungasha virago wowote, kufuatia uongozi wa klabu hiyo kumkata mshahara wake.
Habari kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, kitendo hicho kilimfanya Niyonzima agome kusafiri na timu hiyo kwenda Arusha kwa ajili ya pambano la ligi dhidi ya JKT Oljoro kabla ya kubadili msimamo wake.
Kwa mujibu wa habari hizo, kiongozi mmoja wa juu wa Yanga aliagiza Niyonzima akatwe sehemu ya pesa za mshahara wake kwa ajili ya kufidia pesa alizokopa alipokwenda Rwanda kuichezea timu ya taifa ya nchi hiyo hivi karibuni.
Imedaiwa kuwa, Niyonzima alikopa pesa hizo kwa uongozi kwa ajili ya kuwapelekea wazazi wake.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam juzi, Niyonzima alisema amekerwa na kitendo cha uongozi kuamua kumkata pesa zake zote za mshahara kwa wakati mmoja ajili ya kufidia deni hilo.
Alisema uongozi ulipaswa kutumia busara kwa kumkata pesa hizo kidogo kidogo hadi deni hilo litakapomalizika.
‘Mimi nina familia, ambayo inanitegemea. Uongozi ulipaswa kunichukulia mimi kuwa ni binadamu mwenye familia, siwezi kusafiri nikaiacha familia yangu bila chakula,”alisema.
Niyonzima alisema pia kuwa, upo uwezekano mkubwa wa kugoma kuingia kambini kwa ajili ya kujiandaa kwa pambano lao la mwisho la ligi dhidi ya Simba kutokana na kukerwa na uamuzi huo wa uongozi.
"Hiki ni kitendo cha uonevu. Siwezi kusafiri na kuwaacha mke wangu na watoto wakilala na njaa. Nilimweleza katibu (Selestine Mwesigwa)
lakini alikaidi kufahamu tatizo langu na amesisitiza kwamba ataendelea kukata deni langu,"alisema mchezaji huyo.
Pamoja na kuiwekea ngumu Yanga, Niyonzima amesema hana mpango wowote wa kutaka kujiunga na klabu ya Azam baada ya mkataba wake na Yanga kumalizika.
Alikiri kuwa, mkataba wake na Yanga unatarajiwa kumalizika mwaka 2013 na iwapo kuna timu inamuhitaji, inapaswa kuzungumza na viongozi wa klabu yake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment