KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, April 7, 2012

BURIANI STEVEN KANUMBA


NI pigo kubwa na zito. Si kwa familia ya marehemu Steven Kanumba pekee, bali hata kwa wasanii wa fani ya filamu nchini pamoja na mashabiki wa fani hiyo katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Ni vigumu kuelezea namna kila mtu anayemfahamu Kanumba alivyopokea na kuguswa na taarifa za kifo chake. Wapo walioamini, lakini wengine waliona kama ni ndoto. Wengine walidhani taarifa hizo ni za uzushi.
Kwa wengine, taarifa za kifo cha Kanumba zilionekana kama vile ni za utani. Hawakuamini. Wapo waliopiga simu huku na kule kutaka uthibitisho na wengine walifunga safari hadi nyumbani kwake Sinza, Dar es Salaam.
Taarifa za kifo cha Kanumba zilianza kusambaa saa tisa usiku wa kuakia jana. Kila aliyepata taarifa hizo naye alimtaarifu mwenzake. Baada ya saa chache, asilimia kubwa ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wakawa wamepata taarifa hizo, hasa baada ya kuanza kutangazwa na vituo mbalimbali vya redio na televisheni nchini.
Kanumba (28) alifariki dunia nyumbani kwake Sinza baada ya kudondoka na kujibamiza sakafuni akiwa chumbani kwake. Tukio hilo lilitokea baada ya kuzozana na mpenzi wake, Elizabeth Michael ‘Lulu’.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, kulijitokeza hali ya kutokuelewana kati ya Kanumba na Lulu na kusababisha wagombane. Inasemekana Lulu alimsukuma Kanumba na kugonga kichwa chake chini.
Habari ambazo hazijathibitishwa zimeeleza kuwa, Kanumba alikuwa akioga ili watoke matembezini ndipo alipomsikia Lulu akiongea kwa simu na mtu mwingine na alipotoka kumuuliza, ndipo mzozo kati yao ukaanza.
Mdogo wa Kanumba, ambaye alikuwepo nyumbani usiku huo, Seti alithibitisha kutokea kwa majibizano kati ya kaka yake na Lulu na kuongeza kuwa, binti huyo ndiye aliyempa taarifa za Kanumba kuanguka chumbani kwake.
Seti alisema baada ya kuingia chumbani kwa Kanumba, alimkuta amedondoka sakafuni huku povu likimtoka mdomoni na baadaye wakabaini kwamba alishakata roho. Lulu, ambaye alitoweka nyumbani hapo kutokana na kuchanganyikiwa, anashikiliwa na polisi kwa ajili ya uchunguzi.
Hivyo ndivyo mauti yalivyomkuta Kanumba. Ametangulia kule ambako binadamu wote lazima watafika, lakini kila mmoja kwa siku na muda wake.
Ni kweli kwamba mauti huugeuza mwili wa binadamu ukawa vumbi, lakini yale mema aliyoyafanya hapa duniani yatabaki kuwa kumbukumbu kwa miaka mingi ijayo.
Wasanii wengi wa filamu wameelezea kuguswa mno na kifo cha Kanumba kwa sababu alikuwa mfano wa kuigwa kwao kutokana na mafanikio makubwa aliyoyapata kiusanii katika kipindi kifupi cha maisha yake.
Kwa mashabiki wa filamu za kibongo, Kanumba alikuwa ni namba moja na kwa kiasi kikubwa aliweza kuweka viwango kwani alikuwa anafaa kwa kila kona kuanzia kuigiza mpaka kuvaa.
Kanumba alikuwa akiishi maisha tofauti na wasanii wenzake hivyo kuwavutia watu wa rika zote. Amemaliza kipindi chake cha miaka 28 akiwa ameacha kumbukumbu ambayo itaishi kwa muda mrefu.
Kanumbaa alizaliwa Januari 8, 1984 mkoani Shinyanga. Alipata elimu ya msingi katika shule ya Bugoyi na baadaye sekondari ya Mwadui, kabla ya kuhamia Dar Christian Seminary.
Baada ya kumaliza kidato cha nne Dar Christian, Kanumba alijiunga na sekondari ya Jitegemee, Dar es Salaam kwa ajili ya masomo ya kidato cha tano na sita. Ni wakati huo akiwa Jitegemee, Kanumba alianza shughuli za sanaa katika kundi la Kaole Sanaa Group la Magomeni, Dar es Salaam. Alishiriki kucheza tamthilia nyingi za kundi hilo zilizokuwa zikirushwa hewani na kituo cha televisheni cha ITV kama vileTufani, Gharika, Baragumu na Sikitiko Langu.
Baada ya kukomaa Kaole, Kanumba aliamua kuanzisha kampuni yake mwenyewe ya filamu na hadi anakutwa na umauti, alikuwa mwigizaji anayefahamika Afrika nzima. Baadhi ya filamu alizotunga na kuzicheza na kumpatia umaarufu mkubwa ni pamoja na Haviliki, Dangerous Desire, She is My Sister, Dar 2 Lagos, Cross my Sin, Village Pastor, Family Tears, Johari, Riziki, Deception, The Shock, Uncle JJ, Off Side, More than Pain, Young Billionaire, This is it, Moses, Devil Kingdoma, Because of you na Big Daddy.
Marehemu Kanumba pia aliwahi kushirikiana na baadhi ya wasanii maarufu wa Nigeria kucheza filamu zake. Miongoni mwa wasanii hao ni Ramsey Nouah, Mercy Johnson, Emmanuel France na Nkiru Silvanus.
Enzi za uhai wake, Kanumba aliwahi kushinda tuzo nyingi za filamu ikiwa ni pamoja na mwigizaji bora mwaka 2006 na 2007 na msanii bora wa mwaka 2007 na 2008.
Kanumba hakuwa tu mwigizaji na mtayarishaji maarufu wa filamu. Hivi karibuni aliteuliwa kuwa balozi wa Oxfam Grow kwa Tanzania.
Baadhi ya watu, ambao Kanumba alikuwa akiwataja mara kwa mara na kuwashukuru kutokana na mafanikio aliyoyapata ni pamoja na Chrissant Mhengga, Sharifa Kalala, Mtitu, Sanura Hussein, Vicent Kigosi na wasanii wa kundi la Kaole.
Kanumba atakumbukwa na wengi sana kwa ucheshi wake, upole na ushirikiano mzuri na wenzake katika kazi. Kifo cha Kanumba ni pigo katika tasnia ya filamu Tanzania. Taifa limempoteza mtu ambaye alikwishaanza kuitangaza vema nchi kupitia sanaa hiyo na ambaye angetarajiwa kuitangaza zaidi katika anga za kimataifa kupitia sanaa hii. Wanigeria kwa sasa wanaijua Tanzania kupitia filamu. Vivyo hivyo kwa nchi ya Ghana, ambako Kanumba alikwenda kucheza filamu mwaka jana akiwa na Monalisa.
Nchi nyingi za Afrika zinaijua Tanzania hivi sasa kupitia fani ya filamu na hii ni kutokana na kazi nzuri ya Kanumba. Mwenyewe aliwahi kukaririwa akisema kuwa ndoto yake ni kucheza filamu za Hollywood, ambako aliwahi kutembelea mwaka jana.
Buriani Kanumba. Kifo chako kimeacha pengo kubwa katika tasnia ya filamu. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yako mahali pema.


No comments:

Post a Comment