MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage amejigamba kuwa, wamewaandalia zawadi nzuri wachezaji wao iwapo timu hiyo itatwaa ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara msimu huu.
Rage alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, wamefikia uamuzi huo baada ya kukutana na wachezaji wao mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mwenyekiti huyo wa Simba alisema wameamua kuwaandalia zawadi wachezaji wao ili kuwaongezea ari katika mechi za mwisho za ligi kuu.
"Tulizungumza na wachezaji mambo mengi ya msingi na kuna mambo mazito tuliyowaandalia kwa sababu wamekuwa wakitupa raha sana. Isingekuwa jitihada zao, hali ingekuwa mbaya sana,"alisema.
Simba inaongoza ligi kuu ya Tanzania Bara kwa kuwa na pointi 53 na jana ilitarajiwa kucheza mechi nyingine dhidi ya JKT Ruvu.
Akizungumzia maandalizi ya mechi yao ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Al Ahly Shandy ya Sudan, Rage alisema wameshaanza kujipanga ili kuhakikisha wanashinda pambano hilo.
Pambano kati ya Simba na Shandy limepangwa kuchezwa Aprili 29 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya timu hizo kurudiana wiki mbili baadaye nchini Sudan.
"Siwezi kusema tumepanga kufanya nini katika mechi hiyo, lakini uongozi pamoja na benchi la ufundi tumeshafanya kikao cha kujadili mechi hiyo na pia kupeana majukumu ya kufanya,"alisema.
No comments:
Post a Comment