Na Aboud Mahmoud, Zanzibar
WAAMUZI wanne wa soka wamefungiwa kuchezesha mechi za michuano mbalimbali ya ligi za Zanzibar kwa muda wa mwaka mmoja kwa makosa ya utovu wa nidhamu.
Waliokumbwa na adhabu hiyo ni pamoja na Ramadhani Ibada Kibo na Mgaza Kinduli wanaotambuliwa na Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA). Wengine ni Remtullah Ali na Mohammed Kassim.
Adhabu hizo zilitangazwa juzi na Ofisa Habari wa Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA), Munir Zakaria alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa.
Munir alisema ZFA imefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa, waamuzi hao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu.
“Baada ya kuziadhibu klabu pamoja na wachezaji, tumebaini kuwa baadhi ya waamuzi nao wamekuwa chanzo cha vurugu michezoni, hivyo tumechukua uamuzi wa kuwasimamisha,”alisema.
Ofisa huyo alisema wameamua kutoa adhabu kali kwa waamuzi hao ili liwe fundisho kwa wengine, wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Alisema ZFA imetoa onyo kwa waamuzi wengine wanaochezesha ligi mbalimbali, kuheshimu sheria 17 za mchezo huo, vinginevyo nao watakumbwa na fagio la chuma.
“ZFA imechoshwa na vitendo vya vurugu vinavyotokea katika mechi mbalimbali za ligi, hivyo inatoa onyo kwa waamuzi wazingatie sheria 17 za soka,”alisema.
No comments:
Post a Comment