KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, April 18, 2012

Sistaafu ndondi hadi nipigwe nyakanyaka-Matumla

BONDIA mkongwe wa ngumi za kulipwa nchini, Rashid Matumla 'Snake Boy' amesema hatarajii kustaafu mchezo huo hivi karibuni.
Akihojiwa katika kipindi cha Jambo kilichorushwa hewani na TBC 1 hivi karibuni, Matumla alisema bado hajaona sababu za kumfanya astaafu ndondi hizo.
"Siwezi kustaafu kwa sasa kwa sababu sijaona bondia wa kunisambaratisha,"alisema.
Bondia huyo aliyeweka rekodi ya kutwaa mkanda wa mabara na ubingwa wa dunia wa uzani wa middle alisema, hajawahi kupata kipigo kizito kinachoweza kumfanya aseme sasa basi.
"Sijawahi kupigwa hadi nikachakazwa. Angewahi kutokea bondia wa aina hiyo, ningeshastaafu ngumi miaka mingi iliyopita,"alisema.
Hivi karibuni, Matumla alidundwa kwa pointi na Maneno Osward katika pambano lisilo la ubingwa lililofanyika kwenye ukumbi wa Dar Live, Mbagala, Dar es Salaam.
"Katika ngumi, upo muda wa kustaafu, ukifika nami nitafanya hivyo,"alisisitiza.
Matumla alisema ameshapigana na Maneno mara nyingi na kuongeza kuwa, haoni iwapo ana upinzani mkubwa sana kwake.
Pambano kati ya Matumla na Maneno lilikuwa la tano kuwakutanisha mabondia hao. Matumla ameshinda mapambano matatu wakati Maneno ameshinda mawili.
Kwa mujibu wa Matumla, anatarajia kuzipiga tena na Maneno hivi karibuni mkoani Kilimanjaro.
Alisema ameamua kuzipiga tena na Maneno kwa sababu sheria za ndondi zinaruhusu mabondia kupigana mara zozote na pia iwapo mapromota wataona pambano hilo lina maslahi kwao.
Matumla alisema hahofii sura yake kubadilika kwa sababu ya kukumbwa na ngumi nzito kutoka kwa wapinzani wake kwa sababu hivyo ndivyo mchezo huo ulivyo.
"Katika ndondi, unakwepa na kupiga, mambo ya sura kuharibika ni matokeo,"alisema.
Pamoja na kucheza ngumi kwa miaka mingi, Matumla alisema mchezo huo hauna maslahi makubwa kwa mabondia wa Tanzania na kwamba wanapigana kwa sababu ya kutafuta pesa za kuendesha maisha yao.
Alisema moja ya mikakati yake katika siku zijazo ni kuanzisha shule yake ya ndondi. Alisema anatarajia kuanzisha shule hiyo mkoani Kilimanjaro.
Alimtaja bondia wa ngumi za kulipwa anayemvutia kuwa niFrancis Miyeyusho, ambaye amewahi kupigana mara kadhaa na ndugu yake,Mbwana Matumla.
Matumla, ambaye pia ni mmoja wa viongozi wa kamisheni ya ngumi za kulipwa nchini (TPBC), anaye mtoto wa kiume, ambaye ndiye aliyerithi kipaji chake.

No comments:

Post a Comment