'
Saturday, April 28, 2012
DIAMOND: KUREKODI ALBAMU SASA BASI
MSHINDI wa tuzo tatu za muziki za Kilimanjaro, Naseeb Abdul ‘Diamond’ amesema kuanzia sasa, hatakuwa akirekodi albamu ya nyimbo zake mpya.
Badala yake, Diamond amesema atakuwa akirekodi wimbo mmoja mmoja hadi soko la muziki wa kizazi kipya litakapobadilika nchini.
Diamond alisema hayo mjini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, alipokuwa akilalamikia nyimbo zake kuvuja mara kwa mara kabla ya uzinduzi wa albamu yake.
Msanii huyo mwenye mvuto alisema, amekuwa akikabiliwa na tatizo hilo tangu alipojitosa kwenye muziki huo na ameona njia pekee ya kukabiliana nalo ni kuacha kutoa albamu,
“Kwa sasa hata ukitoa albamu huwezi kuuza kwa sababu nyimbo zote zinakuwa tayari zipo mitaani na kila mtu anakuwa nazo nyumbani kwake,”alisema.
Diamond alisema anashangaa kuona wimbo wake mpya wa Lala salama umeshatapataa kwenye vituo mbalimbali vya redio wakati hajaanza kuusambaza.
Alisema kuvuja kwa wimbo wa msanii na kuanza kupigwa mara kwa mara kwenye vituo vya radio ni tatizo, hasa kibiashara, lakini inakuwa vigumu kuzuia usipigwe na si rahisi kufanya hivyo.
“Nipo nyumbani, nasikia kwenye redio mashabiki wanaomba wimbo wangu mpya na unasikia unapigwa. Natamani kuzuia isipigwe, lakini nashindwa kwa sababu nikifanya hivyo, nitawakorofisha mashabiki wangu,”alisema.
“Kwa upande mwingine, inaonyesha ni jinsi gani nyimbo zako zinavyopendwa na unavyoheshimika kwa sababu sijawaomba wafanye hivyo ama kuwalipa chochote, hii maana yake wanaheshimu na kuthamini kazi yangu, lakini kibiashara inatuweka kwenye wakati mgumu sana,”aliongeza.
Alisema tatizo hilo lilianza kujitokeza tangu aliporekodi wimbo wake wa kwanza wa Nenda kamwambie na kufuatiwa na wimbo wa Mbagala, ambao alisema uliongoza kwa kuvuja mapema kabla hajaanza kuusambaza.
Msanii huyo alisema wimbo wake mwingine wa Moyo wangu haukuvuja kwa sababu watu wenye tabia ya kuzisambaza nyimbo zake bila ridhaa yake hawakufanikiwa kuupata.
Diamond alisema wimbo wa Mawazo nao ulivuja mapema kwa mashabiki, lakini anashukuru kwamba, baada ya kurekodi video yake, ulionekana mpya zaidi.
“Kusema ule ukweli, vitendo hivi vimekuwa vikinikera sana na kuanzia sasa, kurekodi albamu sasa basi,”alisema Diamond.
“Nitakuwa nikitoa nyimbo baada ya nyimbo hadi soko la muziki wetu litakapobadilika. Hii itanisaidia nyimbo zangu zisizagae hovyo mitaani,”aliongeza.
Diamond ameelezea msimamo wake huo siku chache baada ya kushinda tuzo tatu za muziki za Kilimanjaro, ikiwemo tuzo ya video bora ya mwaka kupitia wimbo wake wa Moyo wangu.
Alitwaa tuzo hiyo baada ya kuzibwaga video za Hakunaga ya Suma Lee, Wangu ya Lady JayDee, Ndoa ndoana ya Casim na Bongo Fleva ya Dully Sykes.
Tuzo nyingine alizoshinda Diamond ni ya mtunzi bora wa mwaka, ambapo aliwabwaga Ally Kiba, Mzee Yussuph, Barnaba na Belle 9 pamoja na tuzo ya mtumbuizaji bora wa kiume, baada ya kuwabwaga Ally Kiba, Dully Sykes, Bob Junior na Mzee Yusuph.
"Namshukuru Mungu, wakati mwingine uvumilivu na subira ni mzuri. Mwaka jana sikupata tuzo, nikamshukuru Mungu, nikaongeza bidii, nikafanya kazi nzuri, leo ninachukua tuzo ya tatu sasa hivi," alisema Diamond baada ya kukabidhiwa tuzo ya tatu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment