KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, April 28, 2012

Simba yapania kuwaangamiza Wasudan J'pili


UONGOZI wa klabu ya Simba umejigamba kuwa, umejiandaa vyema kuhakikisha wanashinda pambano lao la awali la raundi ya tatu ya michuano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Al-Ahly Shandy ya Sudan.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wanatarajia kukutana leo kupanga mbinu za mwisho kwa ajili ya kuiangamiza Shandy.
Rage alisema kikao hicho pia kitapanga zawadi watakazowapatia wachezaji iwapo wataishinda Shandy na kuitoa katika mashindano hayo.
Simba na Shandy zinatarajiwa kumenyana Jumapili katika mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kurudiana wiki mbili zijazo mjini Khartoum.
Rage alisema kikao cha leo kitahudhuriwa na vigogo na wafadhili mbalimbali wa klabu hiyo na kitafanyika kwenye hoteli ya Sapphire Court iliyopo Gerezani, Dar es Salaam.
Mwenyekiti huyo wa Simba alisema, pambano lao la Shandy limepangwa kuanza saa 10 jioni na tiketi zitaanza kuuzwa kesho kwenye vituo mbalimbali vya mjini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Rage, kikosi cha Shandy kikiwa na msafara wa watu 30, kinatarajiwa kutoa nchini leo kwa ajili ya pambano hilo na kimepangiwa kukaa kwenye hoteli ya Durban iliyopo Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, uongozi wa Simba umekiri kuwepo nchini kwa mashushushu wa timu ya Al-Ahly Shandy kwa ajili ya kuipeleleza.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema jana kuwa, mashushushu hao waliingia nchini siku tano zilizopita ikiwa ni pamoja na kukagua hoteli ya Durban, ambayo timu hiyo itafikia.
Upo pia uwezekano kwa mashushushu hao kuhudhuria mechi ilizocheza Simba hivi karibuni katika ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya JKT Ruvu na Moro United.
Pamoja na kutuma mashushushu wao, Kamwaga alisisitiza kuwa, lazima timu hiyo ipate kipigo katika mechi yao ya Jumapili.

No comments:

Post a Comment