VIGOGO vya soka nchini, Simba na Yanga vinatarajiwa kushuka tena dimbani wikiendi hii kumenyana na timu za Toto African na Ruvu Shooting katika mechi za ligi kuu ya Tanzania Bara. Wakati Yanga itamenyana na Toto African kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Simba itavaana na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi hizo mbili zinatarajiwa kuwa na ushindani mkali kwa vile Simba na Yanga kila moja itapania kushinda ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa.
Ligi hiyo ilisimama kwa muda kutokana na Simba kushiriki katika michuano ya kimataifa.
Simba inaongoza ligi iyo kwa kuwa na pointi 50 baada ya kucheza mechi 22, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 47 kutokana na idadi hiyo ya michezo. Yanga ni ya tatu kwa kuwa na pointi 43 baada ya kucheza mechi 21.
Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliipoka Yanga pointi tatu na mabao matatu ilizopata kwa kuishinda Coastal Union bao 1-0 baada ya kupatikana na hatia ya kumchezesha beki Nadir Haroub anayedaiwa alikuwa na kadi nyekundu kwa kosa la kupigana.
Hata hivyo, Yanga imekata rufani kwa kamati ya nidhamu na usuluhishi ya TFF, ikipinga uamuzi huo wa kamati ya ligi.
Kwa mujibu wa ratiba, ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena Jumamosi wakati Polisi itakapoikaribisha Azam mjini Dodoma, JKT Ruvu watakuwa wageni wa Mtibwa mjini Morogoro, Kagera Sugar itaikaribisha African Lyon mjini Bukoba wakati Moro United itacheza na JKT Oljoro.
Mechi nyingine kati ya Villa Squad na Coastal Union itachezwa Jumapili kwenye uwanja wa Chamazi mjini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment