KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, April 18, 2012

Mashauzi awapa tano waandaaji tuzo za Kili

MWIMBAJI nguli wa muziki wa taarab nchini, Isha Ramadhani ‘Mashauzi’ amewapongeza waandaaji wa tuzo za muziki za Kilimanjaro kwa kufanya mabadiliko makubwa katika utoaji wa tuzo.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Isha alisema wasanii waliopata tuzo mwishoni mwa wiki iliyopita walistahili kutokana na maudhui ya nyimbo zao na pia kukubalika na mashabiki.
Isha, ambaye ameshinda tuzo ya wimbo bora wa taarab wa mwaka kupitia kibao chake cha ‘Nani kama mama’ alisema, ni vyema mwanamuziki apate tuzo kutokana na muziki wake kufanya vizuri na pia kukubalika kwake na mashabiki badala ya kubebwa.
“Kusema kweli, safari hii yapo mabadiliko makubwa na waandaaji wamejitahidi sana kurekebisha dosari zilizokuwa zikijitokeza miaka iliyopita,”alisema.
Mwanamama huyo anayemiliki kundi la taarab la Mashauzi Classic alisema, anaamini kilichomwezesha kushinda tuzo za mwaka jana ni kukubalika kwake na mashabiki wa muziki huo.
“Mwaka jana nilikerwa sana na utoaji wa tuzo hizo kwa sababu wimbo wangu wa ‘Mama nipe radhi’ ulikuwa na maudhui mazuri kuliko nyimbo zingine zilizoshindanishwa na ulipendwa sana na mashabiki.
“Siku zote wimbo mzuri hauchoshi kuusikiliza na wala hauchujiki kwa miaka elfu. Nyimbo za mapenzi zinachosha. Kama ni mapenzi yalianza tangu enzi za Adamu na Hawa na hadi leo watu wanazungumzia mapenzi. Lakini kuna vitu hata vikikaa miaka hamsini, ujumbe wake haufi,”alisema mwanamama huyo mwenye mwili tipwatipwa.
Isha alisema amepata faraja kubwa kuwa miongoni mwa washindi wa tuzo hizo na kuongeza kuwa, lengo lake ni kutunga nyimbo zenye mwelekeo tofauti na masuala ya mapenzi.
Alimshukuru mama yake mzazi, Rukia Juma na kiongozi msaidizi wa Mashauzi Classic, Thabiti Abdul, ambao amewauelezea kuwa wamekuwa msaada mkubwa kwake kimuziki.
Vilevile amewapongeza mashabiki wa muziki huo kwa kumpigia kura nyingi na kusema kuwa, bila wao asingeweza kupata mafanikio aliyonayo sasa.
Hii ni mara ya tatu kwa Isha kushiriki kwenye tuzo hizo. Mwaka juzi alishindanishwa kupitia kibao cha Ya wenzenu midomo juu alichokiimba na kundi la Jahazi na mwaka jana alishiriki kupitia kibao cha Mama nipe radhi.

No comments:

Post a Comment