Mabingwa watetezi wa michuano ya Copa Coca-Cola, Kigoma wameng’oka katika michuano ya mwaka huu baada ya kulala mabao 2-1 mbele ya Mara katika mchezo uliochezwa leo (Julai 7 mwaka huu) Uwanja wa Tanganyika Packers ulioko Kawe, Dar es Salaam.
Hadi kipindi cha kwanza cha mechi hiyo ya kutafuta tiketi ya kucheza robo fainali kinamalizika, Mara walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa dakika ya 21 na George Martime.
Kipindi cha pili kilianza kwa nguvu ambapo Mara walifanikiwa kupachika bao la pili dakika ya 52 kupitia kwa Israel Daud. Kigoma ilipata bao lake dakika ya 63 mfungaji akiwa Hassan Ramadhan.
Kwa ushindi huo sasa Mara itacheza mechi ya robo fainali Julai 10 mwaka huu saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Karume na mshindi wa mechi kati ya Morogoro na Pwani itakayochezwa leo jioni kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers.
Nayo Temeke imepata tiketi ya kucheza robo fainali baada ya leo kuitoa Ruvuma kwa mikwaju ya penalti katika mechi ya 16 bora iliyofanyika Uwanja wa Karume. Hadi dakika 90 za kawaida zinamalizika timu hizo zilikuwa zimefungana mabao 2-2.
Katika mikwaju ya penalti, Temeke ambayo itcheza robo fainali Julai 10 mwaka huu saa 2 asubuhi kwenye Uwanja wa Karume na mshindi wa mechi kati ya Mjini Magharibi na Kagera inayochezwa leo jioni kwenye uwanja huo ilipata penalti 3 dhidi ya moja ya wapinzani wao.
Hatua ya 16 bora inaendelea kesho (Julai 8 mwaka huu) kwa mechi nne. Asubuhi Kinondoni itacheza na Rukwa (Uwanja wa Karume), na Dodoma itacheza na Arusha (Uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe).
Mechi za jioni itakuwa Kilimanjaro na Mwanza ambazo zitapambana kwenye Uwanja wa Karume wakati Tabora itaumana na Tanga kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers.
AS VITA, URA KUTUA DAR JULAI 12
Timu za AS Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na URA ya Uganda zinatarajia kuwasili nchini Julai 12 mwaka huu kushiriki michuano ya Klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) itakayofanyika Dar es Salaam kuanzia Julai 14 mwaka huu.
AS Vita Club ambayo iko kundi A pamoja na timu za Simba (Tanzania Bara), Ports (Djibouti) na URA itawasili saa 1.20 usiku kwa ndege ya Kenya Airways ikipitia Nairobi.
Nayo URA itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jioni ya siku hiyo kwa ndege ya Air Uganda. AS Vita imepangiwa kufikia hoteli ya Rombo Green View wakati URA itakuwa hoteli ya Royal Valentino.
No comments:
Post a Comment