KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, April 14, 2013

YANGA YAMTENDEA HAKI MANJI, LEO NI SIMBA NA AZAM



YANGA jana iliendelea kuchanua katika michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuibugiza JKT Oljoro mabao 3-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ushindi huo mnono wa Yanga umekuja siku chache baada ya Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yussuf Manji kukilalamikia kikosi chake kwa kuibuka na ushindi kiduchu wa bao 1-0 katika mechi zake zilizopita za ligi hiyo.

Katika kikao chake na wachezaji, Manji alisema anataka kuiona timu yake ikitoka uwanjani na ushindi mkubwa wa mabao na kuahidi kuwazawadia sh. milioni 100 iwapo watafanikiwa kutwaa ubingwa msimu huu.

Kutokana na ushindi huo, Yanga sasa imefikisha pointi 52 baada ya kucheza mechi 22, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 46. Azam inatarajiwa kushuka dimbani leo kwenye uwanja huo kumenyana na mabingwa watetezi, Simba.

Katika mechi hiyo, Yanga ilijipatia mabao yake yote matatu kupitia kwa Nadir Haroub 'Cannavaro, Simon Msuva na Hamisi Kiiza.

Cannavaro alifunga bao la kwanza baada ya kutokea piga nikupige kwenye lango la JKT Oljoro, kufuatia mpira wa kona uliopigwa na Haruna Niyonzima.

Msuva aliongeza bao la pili baada ya kupokea pasi kutoka kwa David Luhende, akawatoka mabeki kadhaa wa Oljoro kabla ya kufumua shuti kali lililotinga moja kwa moja wavuni.

Bao la tatu lilifungwa na Kiiza baada ya kupokea pasi kutoka kwa Niyonzima na kumpiga chenga kipa wa Oljoro kabla ya kuutumbukiza mpira wavuni.

No comments:

Post a Comment