KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 5, 2012

Waamuzi kituo cha Twalipo waenda Burundi

WAAMUZI 12 wa kituo cha Jeshi cha Twalipo kilichopo Chang'ombe, Dar es Salaam wameondoka nchini kwenda Burundi kwa ajili ya kuchezesha mechi za michuano ya Rolling Stone.
Waamuzi hao waliondoka jana saa 12 asubuhi kwa basi la Muro Coach wakiwa chini ya mkufunzi wao. Stafu Sajenti Abel Kitundu.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwenye kituo cha mabasi cha Ubungo, Kitundu alisema waamuzi hao wanakwenda Burundi kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunzinza.
Kwa mujibu wa Kitundu, vijana hao ndio pekee watakaochezesha mechi za michuano hiyo, inayotarajiwa kuanza kesho mjini Bujumbura.
" Waandaaji wa michuano hiyo walituomba tuwapelekee waamuzi 12 kutoka kituo chetu kwa vile hawataki ichezeshwe na waamuzi wengine,"alisema Kitundu.
Michuano ya Rolling Stone huandaliwa kila mwaka na huzishirikisha timu za vijana wa chini ya miaka 20.
Waamuzi wa kituo cha Twalipo wamekuwa wakipata mafunzo ya uamuzi yanayoandaliwa na mara kwa mara na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ajili ya kuwaendeleza.
Hivi karibuni, vijana 15 wa kituo hicho walishiriki katika mafunzo ya kuchezesha soka yaliyoendeshwa na TFF kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na kufaulu vizuri mitihani yao.
Kwa sasa, vijana hao, ambao pia huchezesha michuano ya Kombe la Uhai na Copa Coca Cola, wameshaanza kufanya mitihani ya uamuzi kwa ajili ya kupangiwa madaraja.

No comments:

Post a Comment