KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, May 30, 2012

P-SQUARE WAFANYA KUFURU









Wanunua ndege ya kusafiria aina ya airbus
Waingizwa kwenye klabu ya mabilionea Nigeria
LAGOS, Nigeria
WANAMUZIKI ndugu wawili mapacha wa kundi la P Square la Nigeria, Peter na Paul Okoye hivi karibuni walidhihirisha kuwa, pesa kwao si tatizo baada ya kununua ndege yao binafsi ya kusafiria.
Habari za uhakika zimeeleza kuwa, peter na Paul wametumia mamilioni ya dola kununua ndege hiyo aina ya airbus kutoka katika moja ya kampuni za Arabuni.
Peter na Paul wanatajwa kuwa ndio wanamuziki tajiri kuliko wote nchini Nigeria kwa sasa, wakiwa wamerekodi na kuuza albamu kadhaa sehemu mbalimbali duniani.
“Tumenunua ndege yetu ya kusafiria. Asante Mungu na mashabiki. Nyote mmewezesha hili lifanikiwe,” alieleza Peter kupitia kwenye mtandao wa Twetter.
Wanandugu hao, ambao wamekuwa wakitengeneza pesa nyingi kupitia muziki, pia wanamiliki mali mbalimbali katika miji ya Jos na Port Harcout, likiwemo jumba la kifahari lenye thamani ya Naira milioni 400 lililopo katika mji wa Lagos.
Wanamuziki hao pia wanamiliki magari ya kifahari aina ya Sequioa Sports Utility Vans (SUVs), Toyota Altima na mengineyo kadhaa.
Wachambuzi wa masuala ya muziki wameeleza kuwa, Peter na Paul kwa sasa wameingizwa kwenye klabu ya mabilionea nchini Nigeria kutokana na uwezo mkubwa wa kipesa walionao.
Historia ya P-Square inaanzia katika shule ya sekondari ya St Murumba, inayomilikiwa na Kanisa Katoliki mjini Jos, Nigeria. Wakiwa shuleni hapo, walijihusisha zaidi masuala ya muziki na ngoma za kiasili na kuanza kuimba nyimbo za wanamuziki maarufu wa Marekani kama vile MC Hammer, Bobby Brown na Michael Jackson.
Baadaye, mapacha hao waliunda kundi lililojulikana kwa jina la MMMPP, ikiwa ni vifupisho vya majina ya Itemoh, Michael, Melvin, Peter na Paul.
Kutokana na kuvutiwa na muziki wa Michael Jackson, waliamua kujikita katika uchezaji wa miondoko ya break dance na kuunda kundi la Smooth Criminals mwaka 1997.
Mwaka 1999, Peter na Paul waliamua kurejea katika shule ya muziki kwa ajili ya kuendeleza vipaji vyao katika upigaji wa kinanda, drums na magita ya besi na rhythm. Nyimbo walizopiga zilitumika katika filamu kadhaa za Kinigeria kama vile Tobi, Mama Sunday, Moment of Bitterness na Evas River.
Mwaka huo huo, mapacha hao waliamua kuunda kundi lao la Double P kabla ya kubadili jina na kujiita P-Square. Kazi zao zinasimamiwa na Bayo Odusami, maarufu zaidi kwa jina la Howie T, promota maarufu nchini Nigeria na Mkurugenzi wa Kampuni ya Adrot Nigeria Limited.
Mwaka 2001, P-Square walishinda shindano la Grab Da Mic na kampuni ya Benson & Hedges iliamua kudhamini albamu yao ya kwanza, inayojulikana kwa jina la Last Nite, iliyotolewa chini ya lebo ya Timbuk2.
Miezi mitatu baada ya kutoa albamu hiyo, kundi la P-Square lilishinda tuzo ya kundi linalochipukia kimuziki barani Afrika katika tuzo za Kira.Pia walishinda tuzo ya kundi bora la muziki wa R&B mwaka 2003.
Mwaka 2005, P-Square walitoa albamu yao ya pili, inayojulikana kwa jina la Get Squared chini ya lebo yao, Square Records. Albamu hiyo ilisambazwa na Kampuni ya TJoe Enterprises. Video za albamu hiyo zilishika namba moja kwa wiki nne mfululizo katika MTV Base.
P-Square wana mashabiki wengi zaidi nchini Afrika Kusini, hasa katika mji wa Cape Town. Wamewahi kufanya maonyesho na wanamuziki mbalimbali maarufu duniani kama vile Ginuwine, Sean Paul, Akon na Busola Keshiro.
Mwaka 2007, kundi hili lilitoa albamu yao ya tatu, ambayo ndiyo inayoongoza kwa mauzo. Albamu hiyo, inayojulikana kwa jina la Game Over, iliuzwa nakala milioni nane sehemu mbalimbali duniani.
Albamu yao ya nne inayojulikana kwa jina la Danger ilitoka mwaka 2009. Ndani ya albamu hiyo, walirekodi baadhi ya nyimbo zao kwa kushirikiana na wasanii wengine nyota kama vile 2face Idibia, J Martins na Frenzy.
Mwaka 2010, kundi hilo lilishinda tuzo ya wasanii bora wa mwaka katika tuzo za Kora zilizofanyika katika mji wa Ouagadougou, Burkina-Faso. Walitangazwa kuwa washindi wa tuzo hiyo wakati wakiwa London, Uingereza walilokwenda kufanya onyesho.

No comments:

Post a Comment