MWANAMUZIKI Jose Mara wa bendi ya muziki wa dansi ya Mapacha Watatu amesema, haamini iwapo ushirikina unaweza kuisaidia bendi kupata mafanikio.
Jose amesema mashabiki wanaweza kuvutiwa na nyimbo za bendi iwapo zimepigwa kwa mpangilio mzuri na mashairi yake yanatoa ujumbe muhimu kwa jamii.
Mwimbaji huyo wa zamani wa bendi ya FM Academia alisema hayo wiki hii mjini Dar es Salaam alipokuwa akijibu swali aliloulizwa iwapo ni kweli mauzo ya albamu za muziki hutegemea zaidi ndumba.
Alisema hana hakika iwapo viongozi wa FM Academia walitumia ndumba kuongeza mauzo ya albamu yao ya kwanza, ambayo ilifanya vizuri zaidi sokoni kuliko zilizofuatia.
“Sikuwahi kuwa kiongozi FM Academia, hivyo kama jambo hilo lilifanyika, liliwahusu wao, mimi sikushiriki kabisa, ndio kwanza nasikia kutoka kwako,”alisema mwimbaji huyo mwenye sauti yenye mvuto.
“Lakini binafsi naamini kuwa, ukiimba kitu kizuri, lazima mashabiki watakikubali, lakini siamini kabisa mambo ya ushirikina,”aliongeza.
Jose pia alikanusha madai kuwa, mmiliki wa bendi ya Twanga Pepeta International, Asha Baraka amekuwa na bifu na bendi ya Mapacha Watatu.
Alisema kama kweli kuna bifu kati yao, bifu hilo ni la kibiashara zaidi kwa sababu Asha hawezi kuchukia kutokana na wanamuziki wake kuhama na kujiunga na bendi zingine.
Hata hivyo, Jose alisema wakati mwingine, bifu kati ya bendi za muziki zimekuwa zikianzishwa na kukuzwa na vyombo vya habari bila ya wanamuziki kufahamu lolote.
Bendi ya Mapacha Watatu inamilikiwa na Jose, aliyetokea FM Academia na Kalala Junior na Khalid Chokoraa waliotokea Twanga Pepeta.
Jose alisema wasanii wanatakiwa kuwa waangalifu katika kazi zao kwa sababu wanapaswa kuwa na maisha yao wenyewe, hivyo wanapopata mwanya ama malisho mazuri, hawatakiwi kulaza damu.
“Waswahili wanasema, ujinga wa ujanani ni umaskini wa uzeeni,”alisema Jose.
Kwa sasa, Jose ameamua kuacha kabisa kunywa pombe. Alifikia uamuzi huo tangu mwaka jana kwa lengo la kutunza sauti na afya yake.
Alikiri kuwa, wimbo wake wa Buriani Mama ni tukio la kweli. Alisema aliimba wimbo huo kwa lengo la kumuenzi marehemu mama yake na kwanza hata kaburi lililotumika kwenye video ya wimbo huo ni la mama yake.
No comments:
Post a Comment