MWILI wa kiungo wa kimataifa wa Rwanda na klabu ya Simba, Patrick Mafisango ulizikwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye makaburi ya Kinkole yaliyopo nje kidogo ya Jiji la Kinshasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Mafisango alifariki dunia kwa ajali ya gari, usiku wa kuamkia Alhamisi iliyopita katika maeneo ya Chuo cha Ufundi (VETA), Chang'ombe, Dar es Salaam, akiwa anatoka matembezini katika klabu ya Maisha. Gari lake liliacha njia na kutumbukia mtaroni wakati akimkwepa dereva wa pikipiki.
Kifo cha Mafisango kimeacha simanzi kubwa kwa wanachama, viongozi na mashabiki wa Simba. Pia kimeacha simanzi kubwa kwa mashabiki wa soka wa Rwanda, ambako alikuwa ameitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo, Amavubi Stars.
Mafisango ni mzaliwa wa DRC, lakini alichukua uraia wa Rwanda kwa sababu ya soka. Hakuwahi kucheza soka na kupata umaarufu alipokuwa DRC. Alivipata vyote hivyo baada ya kwenda Rwanda kucheza soka ya kulipwa.
Mwanasoka huyo kipenzi cha wana-Msimbazi alifariki dunia katika kipindi, ambacho klabu yake ilikuwa ikimuhitaji zaidi kwa ajili ya michuano ya ligi na mechi za kimataifa. Alikuwa kipenzi cha wachezaji wenzake, viongozi na hata mashabiki wa Simba.
Ni kweli kwamba Mafisango alikuwa na matatizo yake binafsi na ndio sababu uongozi wa Simba uliwahi kumsimamisha, lakini kutokana na umuhimu wake kwenye kikosi cha timu hiyo, alisamehewa na kuendelea kupiga mzigo.
Kwa wanaofuatilia soka ya Tanzania kwa makini, bila shaka watakubaliana na safu hii kwamba, Mafisango alikuwa na vituko nje ya uwanja, lakini alipokuwa uwanjani, ilikuwa habari nyingine.
Mafisango aliingia nchini miaka mitatu iliyopita na kusajiliwa na Azam. Lakini baada ya viongozi wa klabu hiyo kuonekana kukerwa na vituko vyake, waliamua kumuuza kwa klabu ya Simba kwa kubadilishana na kiungo, Abdulrahim Humud.
Ni kuanzia hapo Mafisango akaanza kujipatia umaarufu mkubwa kutokana na kuimudu vyema nafasi yake ya kiungo mkabaji ama kiungo mshambuliaji. Alikuwa mchezaji wa aina ya pekee, ndio sababu alikuwa kipenzi cha mashabiki wa Simba.
Kutokana na kuguswa na kifo chake, viongozi wa Simba, akiwemo Mwenyekiti, Ismail Aden Rage walipatwa na kigugumizi wakati wa kuuaga mwili wake. Wachezaji wenzake walishindwa kujizuia kulia, hasa kipa Juma Kaseja na mshambuliaji Haruna Moshi 'Boban', ambaye alikuwa swahiba mkubwa wa Mcongoman huyo.
Ni wazi kuwa Simba imepoteza mchezaji mzuri na muhimu kwenye kikosi chake na itachukua muda mrefu kumpata mchezaji mwingine wa kuweza kuziba pengo lake.
Kinachosikitisha ni kwamba, viongozi wa Simba hawakumtendea haki Mafisango. Walifanya vizuri kuandaa utaratibu wa kuuaga mwili wake na pia kuusafirisha kwenda DRC kwa mazishi, lakini hakuna kiongozi yeyote wa juu aliyekuwepo kwenye msafara huo.
Kwa mtazamo wangu, mwili wa Mafisango ulipaswa kusindikizwa na aidha Rage ama makamu wake, Godfrey Nyange. Lakini ajabu ni kwamba, uongozi uliamua kumteua Mzee Kinesi kusindikiza mwili huo, akiwa amefuatana na Boban.
Hili ni kosa kubwa. Uongozi wa Simba ulipaswa kumpa heshima mchezaji huyo kwa kiongozi wake mmoja wa ngazi ya juu kuusindikiza mwili wake na kuukabidhi kwa wazazi wake. Sielewi ni hofu gani waliyokuwa nayo viongoziSimba hata wakashindwa kufanya hivyo. Ni pia sielewi ni dharura ipi iliyowafanya wasiende DRC kumsindikiza mchezaji wao kipenzi.
Waswahili wana msemo usemao, thamani ya mtu huonekana pale tu anapokuwa hai duniani. Akishafariki basi na thamani yake nayo inakuwa imekwisha.
Nawapongeza sana Simba kwa kuandaa utaratibu mzuri wa kuuaga mwili wa Mafisango, lakini sikubaliani na kisingizio chochote kitakachotolewa kwa nini mmoja wao alishindwa kuusindikiza mwili wa mchezaji huyo kwao. Nawapongeza pia viongozi wa Simba kwa uamuzi wao wa kutotumia tena jezi namba 30 iliyokuwa ikivaliwa na Mafisango kwa lengo la kumuenzi mchezaji huyo, lakini nadhani bado kuna kitu kingine kinachopaswa kufanywa ili kuienzi familia yake.
Kwa mtazamo wangu, nadhani ni vyema viongozi wa Simba waandae mechi maalumu ya kimataifa ya soka ili kuchangisha fedha kwa ajili ya kuisaidia familia yake, hasa watoto wake watatu, ambao bado wadogo na bila shaka wanahitajika kusoma.
Nina hakika hiyo itakuwa njia nyingine nzuri zaidi ya kumuenzi Mafisango na kuwafanya wazazi na ndugu zake waiheshimu Simba na Tanzania kwa jumla. Mechi hiyo pia itawafanya wazazi na ndugu wa Mafisango waone mtoto wao hakupotea njia kuja kucheza soka Tanzania.
Njia nyingine nzuri ya kumuenzi Mafisango ni kwa wachezaji wa timu hiyo kucheza kwa kujituma kama alivyokuwa akifanya kiungo huyo, ambaye kila alipofanya kosa uwanjani lililoigharimu timu yake, alifanya kila njia kujirekebisha na kuwapa furaha mashabiki wa timu hiyo.
No comments:
Post a Comment