'
Saturday, May 12, 2012
TP MAZEMBE WAFANYIWA VURUGU SUDAN
MASHABIKI wa klabu ya Al Merreikh ya Sudan wameufanyia fujo msafara wa klabu ya Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mjini Khartoum, wakidai na wao walipokewa vibaya na klabu hiyo mjini Lubumbashi wiki mbili zilikzopita.
Mazembe yenye washambuliaji wawili Watanzania, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu ipo Khartoum kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Merreikh, hatua ya 16 Bora.
Katika vurugu hizo, basi walilokuwa wamepanda wachezaji wa Mazembe limevunjwa vioo na athari zaidi ikiwemo hali hali za wachezaji bado hazijajulikana.
Sasa mechi hiyo iliyopangwa kufanyika kwenye Uwanja wa Omdurman, hatima yake ipo mikononi mwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF)- ambayo inatarajiwa kuchukua hatua muda mfupi ujao, kubwa zaidi ikitarajiwa kuifuta mashindanoni Merreikh na kuifungia hivyo Mazembe kusonga mbele.
Katika mchezo wa kwanza, Samatta, maarufu kama Sama Goal, aliibuka shujaa kwenye Uwanja wa Kibassa Maliba, baada ya kufunga bao moja katika ushindi wa 2-0.
Kama ilivyokuwa dhidi ya Power Dynamos, safu ya ushambuliaji ya Mazembe inayoundwa na wakali kama Tressor Mputu, Given Singuluma, Kalaba na Samata ilikuwa mwiba mkali.
Mazembe ilipata kona sita wakati wapinzani wao hawakupata hata moja na katika kona hizo ni moja tu iliyozaa matunda kwa Sama Goal kufunga dakika ya 22 kwa kichwa akiunganisha kona iliyochongwa na Mputu.
Hadi dakika 45 za kwanza zinamalizika Mazembe inayofundishwa na Lamine Ndiaye ilikwenda kupumzika ikiwa inaongoza kwa bao hilo moja tu.
Nahodha Tressor Mputu aliifungia Mazembe bao la pili dakika ya 70, akipiga shuti zuri nje ya eneo la penalti na mpira kutinga nyavuni upande wa kulia wa lango.
Hakuna kilichobadilika katika dakika 20 za mwisho, licha ya nafasi kadhaa zilizoshindikana kutumiwa vema.
Samatta, Mtanzania aliyetokea Simba SC kujiunga na Mazembe katikati ya msimu uliopita, sasa ana mabao mawili katika Ligi ya Mabingwa ndani ya mechi mbili.
Awali alifunga katika sare ya 1-1 na Power Dymanos ya Zambia, mchezo wa kwanza hatua ya 32 Bora, lakini sikku hiyo aliumia bega na akakosa mechi ya marudiano.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment