'
Friday, May 18, 2012
Miembeni yauzwa kwa Mundu
KLABU ya soka ya Miembeni United ya Zanzibar imetangaza kuuvunja rasmi uongozi wake na kuiuza timu hiyo kwa klabu ya Mundu.
Uamuzi wa kuiuza Miembeni umekuja siku chache baada ya kumalizika kwa michuano ya ligi kuu ya Zanzibar. Mundu ni miongoni mwa timu zilizoshuka daraja.
Hafla ya kuiuza Miembeni ilifanyika mwanzoni mwa wiki hii kwenye ukumbi wa Elimu Mbadala, Rahaleo na kuhudhuriwa na viongozi wa juu wa klabu hizo.
Mmoja wa viongozi wa Miembeni, Haji Sultani Tembe aliithibitishia Burudani kuhusu kuuzwa kwa timu hiyo na kulazimika kuuvunja uongozi wake.
Tembe alisema pia kuwa, kutokana na uamuzi huo, wachezaji wote wa Miembeni kwa sasa wapo huru na wanaweza kusajiliwa na timu yoyote.
Katibu Mkuu wa Mundu, Mussa Diku alikiri klabu yake kuinunua Miembeni baada ya kufikiwa kwa makubaliano kati ya viongozi wa pande hizo mbili.
Diku alisema bado wanaendelea na taratibu zingine ili timu hiyo iweze kushiriki tena katika michuano ya ligi kuu msimu ujao.
Uchunguzi wa Burudani umebaini kuwa, uamuzi wa kuiuza Miembeni umelenga kutoa nafasi kwa mkurugenzi wake, Amani Ibrahim Makungu kugombea urais wa Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA).
Chanzo cha habari kimeeleza kuwa, mipango imeanza kufanyika ili kumwezesha Makungu kushika wadhifa huo baada ya kujiuzuli kwa rais wa zamani wa chama hicho, Ali Ferej Tamim.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment