'
Thursday, May 3, 2012
Milovan, Stewart wawafunika makocha wazalendo
SAFARI ndefu ya kusaka ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2012/2013, inatarajiwa kufikia tamati keshokutwa huku timu za Simba na Azam zikiwa na nafasi kubwa ya kutwaa taji hilo.
Katika mechi za mwisho zitakazochezwa keshokutwa, Simba itamenyana na watani wao wa jadi Yanga kwenye Uwanja wa Taifa wakati Azam itavaana na Kagera Sugar kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Simba na Azam zitashuka dimbani zikiwa zimetofautiana kwa pointi tatu. Simba inaongoza kwa kuwa na pointi 59 wakati Azam ni ya pili kwa kuwa na pointi 56.
Iwapo Simba itaifunga Yanga ama kutoka nayo sare, itatwaa taji hilo, lakini iwapo itateleza kwa kufungwa na wakati huo huo Azam kuifunga Kagera Sugar, taji hilo linaweza kubaki Chamazi.
Itakachotakiwa kufanya Azam ni kuifunga Kagera Sugara mabao zaidi ya mawili kwa vile timu hiyo inatofautiana na Simba kwa mabao mawili ya kufunga. Simba imefunga mabao 42 wakati Azam imefunga mabao 40. Kila moja imefungwa mabao 12.
Wakati ligi inatarajiwa kufikia tamati keshokutwa, baadhi ya makocha wa kigeni wameonekana kuzipa mafanikio timu zao huku makocha wazalendo wakishindwa kuonyesha makali yao.
MILOVAN CIRKOVIC
Ni kocha aliyeipa Simba mafanikio makubwa, si tu katika ligi, bali hata michuano ya Kombe la Shirikisho, ambapo timu hiyo imefuzu kucheza hatua ya 16 bora.
Kocha huyo kutoka Serbia pia amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuibadili Simba kimchezo, ambapo sasa inacheza soka ya kuvutia zaidi ikilinganishwa na ilivyokuwa ikicheza katika mzunguko wa kwanza.
Awali, wachezaji wa Simba walikuwa wakichoka haraka hasa katika kipindi cha pili. Haikuwa na uwezo wa kucheza kwa kasi katika dakika zote 90. Lakini hivi sasa, kadri dakika zinavyosonga mbele, kasi ya Simba imekuwa ikizidi kuongezeka.
Cirkovic pia aliiongoza vyema Simba kuzitoa Kiyovu ya Rwanda katika mechi ya raundi ya kwanza ya michuano ya Kombe la Shirikisho kabla ya kuitupa nje ES Setif ya Algeria katika raundi ya pili.
Kocha huyo pia ameiweka Simba kwenye mazingira mazuri ya kusonga mbele baada ya kuiongoza vyema kuichapa Al-Ahly Shandy ya Sudan mabao 3-0 katika mechi ya awali ya raundi ya tatu iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Dar es Salaam. Timu hizo zitarudiana wiki mbili zijazo nchini Sudan.
Iwapo Simba itatwaa ubingwa wa ligi kuu, ni wazi kuwa Cirkovic naye atatwaa tuzo ya kocha bora kwa kuiwezesha timu hiyo kuibuka mabingwa.
Mafanikio mengine ya Simba katika ligi hiyo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na umahiri wa kipa Juma Kaseja, ambaye ameweka rekodi ya kucheza mechi zote na kufungwa mabao 12.
STEWART HALL
Ni kocha mwingine wa kigeni, aliyeleta changamoto kubwa katika ligi hiyo msimu huu na kutoa ushindani mkali kwa timu kongwe za Simba na Yanga.
Azam ndiyo timu pekee iliyoweka rekodi ya kuzishinda Simba na Yanga katika ligi hiyo, ikiwa ni pamoja na kutwaa kombe la Mapinduzi katika michuano iliyofanyika Zanzibar mapema mwaka huu.
Kocha huyo ndiye aliyeziweka Simba na Yanga roho juu katika mbio za kuwania ubingwa na nafasi ya pili kwa kuzitenganisha timu hizo kongwe kutoka nafasi ya kwanza na ya tatu.
Azam sasa ina uhakika mkubwa wa kushika nafasi ya pili na hata kutwaa ubingwa iwapo Simba itateleza na hivyo kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.
Mafanikio ya Azam katika ligi hiyo msimu huu yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na kusajiliwa kwa nyota kadhaa wa kigeni kutoka Ivory Coast, akiwemo mshambuliaji machachari Kipre Tchetche.
Azam ni miongoni mwa timu zinazoundwa na wachezaji wengi wazuri na kwa sasa hakuna shabiki anayeweza kushangaa iwapo timu hiyo itazifunga Simba au Yanga kwenye ligi ama michuano mingine yoyote.
Mabao 16 aliyofunga Boko ni heshima kubwa kwa Azam na kocha wake, Hall na bila shaka tuzo ya mfungaji bora itatua tena kwa mshambuliaji huyo mrefu na tegemeo kubwa la Taifa Stars.
Azam ni timu pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki kuwa na kituo cha michezo chenye ubora wa hali ya juu cha Chamazi huku uwekezaji wake ukiendelea kufanyika kwa awamu na inategemewa na wengi kutikisa kwenye soka la Afrika kama ilivyo kwa TP Mazembe.
Tayari bodi ya wakurugenzi ya Azam FC imeweka wazi kuwa, dhamira ya kuanzishwa kwa klabu hiyo ni kuondoa dhana kuwa watanzania hawawezi na stahili yao ni jina la ‘kichwa cha mwenda wazimu’.
Uongozi wa Azam umedhamiria kugeuza hali hii na kuifanya Tanzania iwe nchi ya kuogopwa na kuheshimika kwenye soka la Afrika. Lakini ili kufikia malengo hayo, inahitaji muda na pia kuungwa mkono na wadau.
KOSTADIN PAPIC
Ni kocha aliyerejeshwa Yanga kimizengwe baada ya kutimuliwa kocha wa zamani wa timu hiyo, Sam Timbe kutoka Uganda, ambaye aliiwezesha kutwaa taji la ligi kuu msimu uliopita na Kombe la Kagame.
Awali, Papic aliletwa Yanga kwa ajili ya kuziba pengo la Dusan Kondic msimu wa 2010/2011, lakini alilazimika kufungasha virago mapema baada ya kushindwa kuelewana na viongozi.
Kurejeshwa kwake Yanga kulisababisha mashabiki wa klabu hiyo wagawanyike, baadhi wakiunga mkono na wengine wakipinga kwa madai kuwa, hakuwa na jipya.
Hata hivyo, Papic ameshindwa kukidhi kiu ya mashabiki wa Yanga kutokana na kutoiletea mafanikio makubwa. Mbaya zaidi, kocha huyo kutoka Serbia amekuwa akitoa kauli za mara kwa mara za kuwashutumu viongozi kwa kushindwa kuihudumia timu vizuri.
Hivi karibuni kocha huyo alikaririwa na vyombo vya habari akilalamikia kutolipwa mishahara yake ya miezi miwili, lakini kauli hiyo ilipingwa vikali na uongozi, ambao ulidai kuwa alishachukua malipo ya awali.
Pengine kilichotibua mipango ya Papic ni kitendo cha wachezaji watano wa Yanga kufungiwa kucheza mechi kadhaa kwa kosa la kumpa kipigo mwamuzi Israel Nkongo na pia kupokwa pointi ilizopata kwa kuifunga Coastal Union baada ya kumchezesha beki Nadir Haroub Cannavaro aliyekuwa na kadi nyekundu.
Tayari kocha huyo ameshamaliza mkataba wake wa kuinoa Yanga na upo uwezekano mkubwa kwa timu hiyo kuwa chini ya kocha mwingine msimu ujao.
TOM OLABA
Unaweza kumwita kocha kijana wa kigeni, aliyemudu kutoa upinzani mkali katika ligi kuu ya msimu huu licha ya kushindwa kutimiza malengo aliyokusudia ya kutwaa ubingwa.
Olaba ameweza kuhimili purukushani za ligi hiyo hadi timu yake kushika nafasi ya tatu. Lakini ni wazi kuwa, makali ya Mtibwa Sugar yameanza kupungua kwa kiasi kikubwa, tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Katika mechi 25 ilizocheza hadi sasa, Mtibwa imeshinda mechi 10,
imetoka sare sita na kupoteza tisa. Imefunga mabao 32, imefungwa mabao 29 na imeambulia pointi 37.
Ni wazi kuwa, iwapo Olaba anataka kuwa na kikosi imara, anapaswa kusajili wachezaji wazuri zaidi msimu ujao, hasa vijana kwa vile wachezaji wengi waliopo sasa wameanza kuzeeka.
JAMHURI KIHWELU ‘JULIO’
Ni kocha aliyekabidhiwa jukumu la kuifundisha Coastal Union baada ya kuondoka kwa Hafidh Badru, ambaye alishindwa kuhimili mikiki mikiki ya ligi kuu.
Julio alileta mageuzi makubwa ndani ya Coastal Union kiasi kwamba timu hiyo ilianza kucheza kwa kujiamini na hatimaye kujinasua katika janga la kuteremka daraja.
Licha ya kuikimbia timu hiyo na kutimkia Arabuni baada ya raundi ya kwanza kumalizika, Julio alirejea nchini na kufufua tena matumaini ya timu hiyo kubaki ligi kuu baada ya kuiwezesha kufanya vizuri katika mechi kadhaa za mzunguko wa pili.
Hadi sasa, Coastal Union inashika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 36 baada ya kucheza mechi 25. Imeshinda mechi 11, imetoka sare mechi tatu na kupoteza 11. Imefunga mabao 28 na kufungwa 29.
SALUM MAYANGA
Alianza kuinoa Kagera Sugar msimu huu akitokea Mtibwa Sugar. Ni kocha aliyerithi mikoba ya George Ssemogerere kutoka Uganda, ambaye aliamua kufungasha virago msimu uliopita.
Kocha huyo ameonyesha uwezo mzuri wa kuiongoza timu hiyo na huenda akapewa tena jukumu hilo msimu ujao. Lakini changamoto kubwa inayomkabili ni kusajili wachezaji wengine wapya.
Kagera Sugar ya sasa siyo ile iliyokuwa ikitamba miaka ya nyuma na kutoa upinzani mkali kwa vigogo vya soka nchini, Simba na Yanga. Makali ya Kagera Sugar yamepungua.
Licha ya kuilazimisha Simba kutoka nayo sare katika mzunguko wa pili na kuichapa Yanga bao 1-0 mjini Bukoba, bado Kagera Sugar inahitaji kusukwa upya ili kuongeza ushindani katika ligi.
Hadi sasa, Mayanga ameiwezesha Kagera Sugar kushika nafasi ya sita katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 32 baada ya kucheza mechi 25.
CHARLES KILINDA
Msimu huu Kocha Charles Kilinda ameendelea kuihakikishia timu hiyo kubaki ligi kuu msimu ujao baada ya kuwa katika nafasi saba za juu.
Katika mechi 25 ilizocheza hadi sasa, imeshinda mechi saba, imetoka sare 11 na kufungwa mechi saba ikiwa imeambulia pointi 32.
Hata hivyo, sifa na heshima ya JKT Ruvu imeporomoka katika msimu huu, kufuatia kubebeshwa mabao mengi katika mechi walizopoteza. Kabla ya mechi za keshokutwa, tayari JKT Ruvu imeshafungwa mabao 32 na kufunga mabao 27.
Ladha ya soka ya maafande hao waliocheza vyema msimu wa 2008/2009 chini ya Kilinda, msimu huu haikuonekana kabisa. Huenda tatizo la majeruhi linaweza kuwa kikwazo kwa kocha huyo, aliyewahi kucheza katika timu ya Yanga miaka ya nyuma.
Katika baadhi ya mechi za mzunguko wa kwanza, Kilinda alisema majeruhi waliharibu malengo yake na katika mzunguko wa pili walikuwa nyanya zaidi kwa kupoteza mechi nyingi.
Huenda mazoea ya kukaa miaka mingi na wachezaji bila ya kuwaondoa au kuongeza damu changa, imechangia kikosi hicho kuyumba katika ligi hiyo iliyokuwa na ushindani mkubwa.
Kilinda hajafanya vibaya sana kiasi cha kutajwa hafai, isipokuwa anatakiwa kufanya mabadiliko makubwa ya wachezaji kwa nia ya kuleta nguvu mpya.
CHARLES BONIFACE MKWASA
Amefanya kazi nzuri ya kuinusuru Ruvu Shooting isishuke daraja, licha ya kukabiliwa na jukumu lingine la kukinoa kikosi cha timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars.
Hadi sasa Ruvu Shooting ipo kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa inashika nafasi ya nane. Inazo pointi 31 baada ya kucheza mechi 25 na haipo kwenye janga la kushuka daraja.
Katika mechi ilizocheza hadi sasa, Ruvu Shooting imeshinda mechi saba, imetoka sare 10 na kupoteza nane, imefunga mabao 22 na kufungwa mabao 21.
Mkwasa alikiri hivi karibuni kuwa, licha ya kutokuwa kwenye nafasi nzuri, kikosi chake kimekuwa kikicheza soka ya kuvutia na ndiyo sababu kimejihakikishia kubaki kwenye ligi hiyo msimu ujao.
ALI KIDI
Ni kocha aliyejijengea jina kubwa katika mechi za mzunguko wa kwanza baada ya timu yake kutwaa uongozi wa ligi mara kadhaa kabla ya kupokonywa usukani.
Kidi aliiongoza JKT Oljoro kushinda mechi nyingi za mzunguko huo na kuonekana tishio kwa vigogo, lakini makali hayo yalipungua mzunguko wa pili na timu hiyo kuanza kupoteza mechi nyingi.
Hadi sasa, JKT Oljoro inashika nafasi ya tisa katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 29 baada ya kucheza mechi 24. Imeshinda mechi saba, imetoka sare nane na kupoteza tisa. Imefunga mabao 17 na kufungwa 24.
ATHUMANI BILALI
Ni kocha aliyerithi mikoba ya Choki Abeid, ambaye naye alirithi mikoba ya John Tegete.
Sifa kubwa aliyonayo Bilali hadi sasa ni kuiongoza Toto African kutoka sare na Simba katika mechi ya mzunguko wa pili iliyochezwa mjini Dar es Salaam kabla ya kuibamiza Yanga mabao 3-2 mjini Mwanza.
Mechi hizo mbili zilifufua matumaini ya Toto African kubaki ligi kuu msimu ujao, lakini kipigo cha mabao 3-1 ilichokipata kutoka kwa Azam, kimeiweka tena kwenye janga la kushuka daraja.
Majaliwa ya Toto African sasa yatategemea matokeo ya mechi yake ya mwisho dhidi ya Coastal Union itakayochezwa mjini Tanga. Sare ya aina yoyote itainusuru timu hiyo kushuka daraja.
Hadi sasa, Toto African inashika nafasi ya 10, ikiwa na pointi 26 baada ya kucheza mechi 25. Imeshinda mechi tano, imetoka sare 11 na kupoteza tisa. Imefunga mabao 24 na kufungwa 30.
JUMANNE CHALE, HABIBU KONDO, HASSAN BANYAI, RASHID CHAMA
Chale ni kocha wa African Lyon, ambayo mwaka jana iliponea kushuka daraja baada ya kufanya vizuri katika mechi za mwisho. Lakini safari hii, Lyon ipo tena mtegoni na iwapo itavurunda mechi yake ya mwisho, huenda ikarejea tena ligi daraja la kwanza.
Vivyo hivyo ndivyo ilivyo kwa Habibu Kondo, ambaye ni miujiza pekee, inayoweza kuinusuru timu yake ya Villa Squad kuepuka kushuka daraja iwapo itafungwa ama kutoka sare katika mechi yake ya mwisho.
Mambo ni mabaya zaidi kwa Hassan Banyai wa Moro United na Rashid Chama wa Polisi Dodoma, ambao timu zao zimeshateremka daraja na mwakani zitacheza ligi daraja la kwanza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment