KLABU ya Coastal Union ya Tanga ipo katika hatua za mwisho za kumsajili kiungo wa kimataifa wa Kenya, Jerry Santo, ambaye pia aliwahi kuichezea Simba.
Ofisa Habari wa Coastal Union, Edo Kumwembe alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, mazungumzo bado yanaendelea kati ya pande hizo mbili.
“Tupo kwenye usajili sasa na tayari tumeishawanasa wachezaji wawili na sasa tupo katika hatua ya mwisho ya kumsajili Jerry Santo,” alisema Edo. Uamuzi wa Coastal Union kumsajili Santo umekuja siku chache baada ya benchi la ufundi la timu hiyo kuamua kuwatema wachezaji tisa walioichezea katika ligi kuu ya Tanzania Bara msimu huu.
Miongoni mwa wachezaji hao ni Ally Ahmed ‘Shiboli’, Benard Mwalala,Ramadhani Wasso, Enock John, Laurent Mugia, Bakari Mohamed, Daudi Changula na Francis Busungu.
Katibu Mkuu wa Coastal Union, El- Siag alisema kwa njia ya simu kutoka Tanga kuwa, miongoni mwa sababu za kuwaacha wachezaji hao ni kushuka kwa viwango vyao.
El-Siag alisema ana matumaini makubwa kwamba, timu hiyo itafanya vizuri zaidi katika msimu ujao wa ligi na kushika nafasi za juu. Katika ligi ya msimu huu, Coastal Union ilishika nafasi ya tano.
Aliwataja wachezaji, ambao tayari wameshawasajili kwa ajili ya msimu ujao kuwa ni Nsa Job kutoka Villa Squad na kiungo Sudy Mohmed wa Toto Africans ya Mwanza.
No comments:
Post a Comment