KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, May 30, 2012

FLAVIANA: Serikali iwathamini wasanii

MWANAMITINDO nyota wa Tanzania, Flaviana Matata ameitaka serikali itambue umuhimu wa kazi za wasanii kutokana na juhudi zao binafsi za kuitangaza nchi kimataifa.
Flaviana amesema itakuwa haina maana kwa msanii kusifiwa kutokana na kazi zake nzuri baada ya kifo chake kama ilivyotokea kwa aliyekuwa msanii nyota wa filamu nchini, marehemu Steven Kanumba.
Akizungumza na mtandao wa filamucentral hivi karibuni, Flaviana alisema kifo cha Kanumba kilionyesha ni jinsi gani wasanii wanavyokubalika katika jamii na hata nje ya mipaka ya Tanzania.
“Tazama wasanii kama AY (Ambwene Yesaya), mtu kama Hasheem Thabeet na wengineo, serikali inawaunga mkono kwa kiwango gani katika kulitangaza Taifa hili? Lakini katika kifo cha Kanumba, tulimwona kila kiongozi alifika msibani,”alisema Flaviana.
Flaviana aliitaka serikali iache kuelekeza nguvu zake katika mchezo wa soka na mingineyo, badala yake itupie macho fani zingine, ambazo zimesaidia kulitangaza jina la Tanzania kimataifa.
Mshindi huyo wa zamani wa taji la Miss Universe Tanzania alisema, licha ya juhudi zake binafsi za kuitangaza nchi kimataifa, alishangazwa kuona akiwekewa vikwazo kugomboa vifaa vya msaada alivyovileta nchini kwa ajili ya abiria wanaosafiri kwa meli.
Flaviana alisema alileta nchini maboya 500 kwa ajili ya msaada kwa wakazi wa kanda ya ziwa, ikiwa ni kumbukumbu ya watu waliopoteza maisha kutokana na ajali ya meli ya MV Bukoba.
“Nilikabiliana na mtihani mkubwa baada ya kuambiwa nilipie kodi mara tano ya bei ya manunuzi,”alisema kwa mshangao mrembo huyo, asiyejichubua wala kubadili rangi ya ngozi yake.
Kanumba alifariki dunia Aprili 7 mwaka huu nyumbani kwake Sinza Vatican, Dar es Salaam na inasemekana kifo chake kilitokana na kusukumwa na msanii mwenzake, Elizabeth Michael ‘Lulu’.

No comments:

Post a Comment